Lugola atoa siku tatu raia wa Msumbiji warejeshwe kwao

Waziri wa mambo ya ndani, Kagi Lugola akiwa katika kijiji cha Kivava halmashauri ya wilaya ya Mtwara alipotembelea eneo walilohifadhiwa raia wa Msumbiji waliokimbia  machafuko nchini humo. Picha na Haika Kimaro

Muktasari:

Raia hao wa Msumbiji waliingia nchini mapema mwaka huu wakivuka mpaka wa Mto Ruvuma baada ya kutokea vurugu katika Kijiji cha Kisungure.

Mtwara.Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola ametaka raia wa Msumbiji waliokimbilia Tanzania, warudishwe nchini kwao ndani ya siku tatusema hali ya usalama nchini shwari, yakiwemo maeneo wanayoishi raia wa Msumbiji waliokimbia uhalifu nchini kwao.

Julai mwaka jana, zaidi ya Watanzania 600 waliokuwa wakiishi Msumbiji na baadhi ya raia wan chi hiyo jirani, walivuka mpaka wa Mto Ruvuma na kuingia Tanzania baada ya kutokea vurugu katika Kijiji cha Kisungure.

Baada ya uhakiki, ilibainika kuwa kati yao, watanzania walikuwa 544 na wengine 92 walikuwa rais wa Msumbiji na mustakabali wa kurejeshwa kwao ulikuwa ukisubiri mazungumzo baina ya serikali za nchi hizi mbili.

Lakini jana, Waziri Lugola alisema hali sasa ni shwari nchini Msumbiji na kuagiza warejeshwe kwao ndani ya siku tatu.

"Isituchukue muda zaidi ya siku tatu tukiwa bado tunahangaika na kikundi cha watu wasiozidi 200 hapa kurudishwa Msumbiji,” amesema waziri huyo ambaye ameanza kasi kwa kishindo baada ya kuteuliwa mapema mwezi huu.

“Warudi (kwao) waendelee na shughili zao. Hatuwezi kuendelea kuwaweka ilhali sisi hatuna kambi ya wakimbizi hapa."

Lugola amesema hayo wakati alipotembelea eneo wanakoishi raia hao wa Msumbiji wapatao 102 katika kijiji cha Kivava wilayani Mtwara.

Waziri Luoga amewaambia watu hao kuwa hawana hadhi ya ukimbizi kwa kuwa Msumbiji hakuna machafuko ya kisiasa, bali ni baadhi ya wahalifu waliofanya matukio yaliyosababisha wakimbie nchi.

"Nimezungumza nao na wamesema wako tayari kurudi nchini kwao kuendelea na maisha yao. Na mimi nakubaliana nao na ndio maana sasa kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa tayari wamejipanga vizuri na sisi vyombo vya usalama na serikali ya mkoa tumejipanga kuhakikisha wanarudi," amesema Kugola

Aidha ameiagiza uongozi wa  mkoa kuhakikisha wanawaangalia kwa makini Watanzanaia wanaorudi kutoka Msumbiji, akisema baadhi yao walienda kinyemela na hivyo Idara ya Uhamiaji haina kumbukumbu zao.

"Watanzania wa namna hiyo lazima tuwaangalie kwa umakini, na katika kuwaangalia hatuwezi tukatumia fedha ambazo Mheshimiwa Rais anahangaika kila siku kuzikusanya maeneo mbalimbali,” amesema.

“Badala ya kuzielekeza kwenye huduma halafu aanze kuzielekeza kwa wenzetu ambao wanatoka nchini kinyemela halafu yanapowakuta kule tuanze kuwalisha na kuwasafirisha? Mheshimiwa mkuu wa mkoa, katika Serikali hii hilo halina nafasi hakuna kumlisha mtu wa aina hii."

Alisema kundi la pili ni Watanzania waliokwenda Msumbiji  kihalali ambao ametaka waangaliwe vizuri kwa kuwa wanaweza pia wahalifu.

“Wapigwe tochi vizuri. Unaweza kuwa umeenda kuhalali lakini bado ni muhalifu. Na wao mkishawapitia vizuri basi waweze kurejea katika maeneo yao," amesema Lugola.

Alitaka vyombo anavyovisimamia kuendelea kufanya shughuli zao katika maeneo wanayoishi raia wa Msumbiji ili kuwabana wahalifu waliokimbia.

"Sisi tunajua kuna watu ambao tunawatafua wanafanya uhalifu maeneo yetu haya (halafu) wamekimbilia Msumbiji,” amesema Lugola.

“Sasa wasije wakatumia fursa hii kurudi huku ndani. Lazima  tukabe maeneo haya, lazima. Hakuna penati itakayopigwa bila kukabwa na anayesimamia chombo chochote kilicho chini yangu, ikitokea hawa ambao wanataka kutumia mwanya wakurudi na badaye ikabainika ni wahalifu na hawakuwachuja vizuri, basi huyo anayesimamia chombo hicho atapata tabu sana.

“Atapata msukosuko yeye huyo ambaye hakusimamia eneo lake vizuri; iwe ni Jeshi la Polisi, Uhamiaji, Magereza, Zimamoto au vitambukisho watapata tabu sana."

Mmoja wa raia waliozungumza mbele ya waziri, Suzan Kolimba ameomba kurejeshwa nchini kwao ili kuendelea na shughuli zao.

Naye Waziri Kolimba amesema wao kama wizara wana wajibu wa kujenga mahusiano mazuri baina ya Tanzania na nchi jirani ya Msumbiji ambayo pia ni nchi marafiki.

"Inapotokea kanzia yoyote ambayo inagusa raia wa kwetu ambao wako kwenye nchi nyingine, sisi kama wizara huwa tunashughulikia hilo jambo kwa karibu zaidi kuhakikisha tunatatua kadhia na changamoto,” alisema Kolimba.

“Ndio maana mnaona niko hapa, lakini pia tuna maafisa wetu wako Msumbiji ili kuhakikisha raia walio Msumbiji kwenye maeneo ambayo kadhia hii imetokea, wanashughilikiwa na kutatuliwa matatizo ambayo yapo,"amesema Kolimba

Raia hao walianza kuingia nchini wakitoka nchini Msumbiji kwa madai ya uwepo wa vurugu ambapo watanzania idadi yao ilikuwa 544 na raia wa Msumbiji walikuwa na 102.