Lukuvi apokewa kwa mabango Ngara

Muktasari:

Wananchi hao walitoa ombi hilo kwa Lukuvi leo Februari 22, 2018 baada ya waziri huyo kufika wilayani humo akitokea  Karagwe akiwa katika ziara ya kiutendaji mkoani Kagera

Ngara. Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amepokewa kwa mabango na wakazi wa Kijiji cha Rwakalemela kilichopo Kata ya Kasulo, Wilaya ya Ngara mkoani Kagera wakimuomba kutatua migogoro ya ardhi.

 

Wananchi hao walitoa ombi hilo kwa Lukuvi leo Februari 22, 2018 baada ya waziri huyo kufika wilayani humo akitokea  Karagwe akiwa katika ziara ya kiutendaji mkoani Kagera

 

Waziri huyo baada ya kufanya kikao cha ndani na viongozi wa wilaya alisikiliza kero za wananchi wa wilaya hiyo kuhusu migogoro ya ardhi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Rwakalemela.

 

Wananchi hao waliokuwa wamebeba mabango yenye ujumbe mbalimbali wa kutaka migogoro ya ardhi kutatuliwa, wengi walimuomba waziri huyo kuwafutia hatimiliki wenye mashamba makubwa waliyoyapata bila kufuata utaratibu wa Sheria ya Ardhi namba 5 ya mwaka 1999.

 

Mmoja wa wananchi hao,  Amiri Rashidi amesema baadhi ya wananchi waliowahi kuwa viongozi wa chama na serikalini na pia wenye uwezo wa kifedha walijimilikisha mashamba makubwa katika kata za Kasulo, Kabanga na  Rulenge na kusababisha wananchi wengine kukosa mashamba.

 

Kitendo cha Rashidi kuzungumza huku akitokwa na machozi kilimwamsha kwenye kiti Ofisa Ardhi wa Wilaya ya Ngara, Betty Munuo kutoa maelezo  kuhusu mzee huyo kwamba, eneo lake alilimiliki mwaka 1969, lakini tangu mwaka 1985 lilichukuliwa na kuwa kituo cha  kuegesha magari.

 

“Huyu anastahili kulipwa tangu mwaka 1985, hivyo anastahili kulipwa na ofisi ya mkurugenzi ambayo haijatekeleza maagizo ya mahakama.

 

Baadhi ya wananchi waliwataja vigogo waliojimilikisha mashamba ambao kutokana na kutowapata majina yao yamehifadhiwa.

 

Awali, Mbunge wa Ngara, Alex Gashaza amesema migogoro ya ardhi wilayani humo ni mingi na wenye uwezo ndio wanaowanyanyasa wananchi masikini.

 

Katika ufafanuzi wake, Lukuvi amesema Serikali inafanya mpango wa kurekebisha utaratibu wa kutatua migogoro ya ardhi kwa kubadilisha mfumo wa mabaraza ya ardhi kwa kila kata.

 

“Migogoro ya ardhi ambayo imefikishwa mahakamani waziri hana mamlaka ya kuingilia, lakini naagiza mwanasheria wa halmashauri hakikisha wajumbe wa mabaraza ya ardhi ambao si waaminifu wanaondolewa kwenye mabaraza hayo ili haki iweze kutendeka,” amesema Lukuvi.