Lukuvi atoa maagizo kwa watendaji Same

Muktasari:

  • Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amesema migogoro ya ardhi inayotokea inasababishwa na watendaji wa wilaya na kuagiza waitafutie ufumbuzi

Same. Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi ameagiza viongozi wote wa halmashauri na wilaya kuhakikisha wanarekebisha mipaka ya vijiji na vijiji ili kutatua changamoto za migogoro ya ardhi katika wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro.

Akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Kwasakwasa vilivyopo Same mjini, leo Jumatatu Novemba 12, 2018, Waziri Lukuvi amesema migogoro mingi ya ardhi imekua ikisababishwa na halmashauri za wilaya.

"Iko migogoro ya ardhi iliyosababishwa na halmashauri za wilaya na nimetoa muda ifikapo Desemba mwaka huu kabla ya uchaguzi migogoro hii iwe imemalizika," amesema Lukuvi.

"Nyinyi halmashauri ndio mnaojua siri ya mipaka yenu, hivyo nawaagiza viongozi wote wa halmashauri na wilaya mrekebishe mipaka ya vijiji ambavyo vina mgogoro," ameongeza.

Pia, Lukuvi amesema wizara yake iko tayari kufuta vyeti vyote vya ardhi ya vijiji wilayani humo endapo wataona ipo haja ya kubadilisha mipaka.

"Sisi tupo tayari kurekebisha hii mipaka upya, haiwezekani wananchi watumie muda mwingi kwenda mahakamani na kupoteza muda kwa sababu ya migogoro hii," amesema Lukuvi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Same, Rosemary Senyamule amesema wilaya hiyo imekua na migogoro mingi ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji na hivyo wilaya hiyo imeendelea kutatua baadhi ya migogoro.

"Tatizo la changamoto tuliyonayo ni fedha ili kuangalia namna ya kupanga matumizi bora ya ardhi, lakini muda sasa umeisha hatujapata fedha hizo," amesema Senyamule.