Lukuvi awapa suluhisho mbadala waliovamia eneo la walimu Dar

Wakazi wa Mbondele, Kata ya Msongola wilayani  Ilala, Dar es Salaam wakiwa na mabango wakati Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi alipotembelea eneo lililokuwa likimilikiwa na walimu zaidi ya 209 ambalo lilivamiwa na wananchi. Picha na Pamela Chilongola

Muktasari:

  • Walimu wataka hukumu ya mahakama kutekelezwa

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amewataka wananchi waliovamia eneo la Mbondole kata ya Msongola kuwalipa haraka wamiliki wa eneo hilo ambao ni walimu mbalimbali zaidi ya 200 ili watafutiwe sehemu nyingine.

Lukuvi alimuagiza kamishna wa ardhi Kanda ya Dar es Salaam na wataalamu kutoka halmashauri ya Ilala kufanya tathmini kujua idadi ya nyumba zilizojengwa eneo la Mbondole linalodaiwa kuvamiwa na wananchi hao.

Pia, aliagiza kamati ya wananchi iundwe ili kujadiliana na walimu 209 ambao ni wamiliki wa eneo hilo, waweze kuchangiwa fedha itakayowasaidia kununua sehemu nyingine.

Eneo hilo lenye eka 210 lina viwanja 342, lilivamiwa mwaka 2009 na wananchi hao hivyo walimu 209 walifungua kesi Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi na kushinda kesi.

“Zaidi ya wananchi 6,000 mliojenga eneo hilo wote ni wavamizi hivyo Serikali inaheshimu uamuzi wa mahakama, kwa sababu kisheria nyumba 2,800 zilizojengwa eneo hilo zilitakiwa zivunjwe,” alisema Lukuvi na kuongeza:

“Kama tungevunja nyumba 2,800 watu wote msingekuwapo na mahakama imempa amri huyu mmiliki avunje nyumba zote, hivyo Serikali hii inatumia njia nyingine mbadala ya kusuluhisha mgogoro huu kwa sababu lengo la walimu ni kujenga nyumba.”

Pia, alisema diwani wa kata hiyo aunde timu ndogo itakayosaidia kuangalia aliyejenga nyumba ya makazi, ili kila mmoja ijulikane kiwango anachotakiwa kuchangia.

“Hiyo timu ndogo itakayoundwa itapita kila sehemu kuangalia viwanja vilivyo wazi ili wakabidhiwe walimu, sitaki kusikia mtu anajenga sehemu iliyo wazi kwa kujenga msingi tutakapoona tutabomoa.

“Mtakapowalipa fedha lazima mlipe gharama ya upimaji wa ardhi waliyopoteza, huwezi ukabomolewa nyumba ya thamani ya Sh7 milioni kwa kushindwa kulipa Sh300,000,” alisema Lukuvi.

Walimu wasimulia

Mratibu wa viwanja hivyo, Sifuni Mbwambo alisema maeneo hayo yalinunuliwa na kupimwa na kutolewa hati viwanja 342 Aprili 17, 2002.

Mbwambo alisema mwaka 2009 viwanja hivyo vilivamiwa, walifuatilia kwa mkuu wa wilaya na kufungua kesi kwenye baraza la ardhi kata ambako walishinda.

Hata hivyo, Mbwambo alisema hukumu hiyo haikutekelezwa na wavamizi hao hivyo mwaka 2017 walifungua kesi katika Mahakama Kuu ya Ardhi na kushinda.

“Wananchi wa eneo hili walienda kwa waziri na kumuomba atuombe walimu kuwa tuwaachie watachanga fedha ili linunuliwe eneo lingine,” alisema Mbwambo na kuongeza:

“Mimi sitaenda tofauti na maelekezo ya mahakama, hivyo binafsi sipo tayari na maombi yenu niliyoyapata na nimekuja hapa kwa ajili ya kumsikiliza waziri ili afanye kitu ili na sisi tupate haki yetu.”