MCL kufanya mabadiliko ya kiutendaji

Mkurugenzi Mtendaji wa MCL, Francis Nanai

Muktasari:

  • Mkurugenzi Mtendaji wa MCL, Francis Nanai amesema hay oleo wakati akizungumza na wafanyakazi wa Mwananchi jijini Dar es Salaam.
  • Amesema kampuni inafanya mabadiliko makubwa ya kimfumo na kiutendaji ili kuwafikishia wateja habari za uhakika zaidi na  kwa haraka kupitia mfumo wa (digitali).

Dar es Salaam. Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL) wachapishaji wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti inafanya mabadiliko ya kiutendaji ili kuendana na mazingira ya soko na uchumi wa hivi sasa.

Mkurugenzi Mtendaji wa MCL, Francis Nanai amesema hay oleo wakati akizungumza na wafanyakazi wa Mwananchi jijini Dar es Salaam.

Amesema kampuni inafanya mabadiliko makubwa ya kimfumo na kiutendaji ili kuwafikishia wateja habari za uhakika zaidi na  kwa haraka kupitia mfumo wa (digitali).

Amesema kuwa kampuni hiyo pia inafanya mabadiliko makubwa katika maeneo ya kubana matumizi katika maeneo mbalimbali ya kiuendeshaji, kusimamisha ajira zilizokuwa zimeidhinishwa kwa mujibu wa bajeti ya kampuni ya mwaka 2016/2017 na kupunguza matumizi katika bajeti ya mafunzo na maendeleo ya wafanyakazi.

Maeneo mengine yenye mabadiliko ni kupunguza safari za mafunzo na kikazi na kusitisha kuongeza mishahara kwa mwaka 2017.

“Sote tunafahamu kuwa Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kurekebisha uchumi na kusukuma gurudumu la maendeleo. Moja ya hatua hizo kubwa ni kubana matumizi ya Serikali kwa njia mbalimbali ikiwamo matangazo ya Serikali na taasisi zake kwenye vyombo vya habari,”amesema

Amesema MCL ikiwa ni chombo cha habari imeathirika na hatua hiyo kutokana na kwamba  duniani kote biashara ya magazeti inategemea kwa kiasi kikubwa mapato yatokanayo na matangazo.

Nanai amesema kutokana na hali hiyo, kampuni italazimika kupunguza baadhi ya wafanyakazi kutoka idara mbalimbali kwa kuzingatia taratibu zote za kisheria, sera za kampuni, haki na msingi wa utu.

“Tunawahakikishia wasomaji, watamaji wa mitandao yetu ya digitali, watangazaji na wananchi kwa ujumla kwamba tutaendelea kutoa habari za uhakika kupitia magazeti yetu na mitandaoni,”alisema.