MSD yazindua mfuko maalumu kwa wajawazito

Muktasari:

Mfuko huo una vifaa 12 ikiwamo  pamba kubwa, mpira wa kuzuia uchafu, taulo ya kike ‘pedi’, glovu, nyembe, kibana kitovu cha mtoto, dawa za kusafishia kidonda na kuogea, mabomba ya sindano mawili na nyuzi za kushonea

Bohari ya Dawa (MSD)  imezindua mfuko wenye vifaa vya kujifungua kwa wajawazito utakaopatikana katika maduka yote ya bohari hiyo na hospitali za umma kwa Sh21,000.

Mfuko huo una vifaa 12 ikiwamo  pamba kubwa, mpira wa kuzuia uchafu, taulo ya kike ‘pedi’, glovu, nyembe, kibana kitovu cha mtoto, dawa za kusafishia kidonda na kuogea, mabomba ya sindano mawili na nyuzi za kushonea.

Akizungumza leo Machi 7, 2018 na waandishi wa vyombo vya habari, Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Laurean Bwanakunu amesema vifaa hivyo ni muhimu mjamzito kuwa navyo anapokwenda kujifungua.

"Serikali imekuwa ikihamasisha kila mama anayekwenda kujifungua awe na vifaa hivyo kwa upande wa MSD, vifaa hivi vinapatikana kwa bei nafuu ambayo kwa mtu wa kawaida anaweza kuimudu ukilinganisha na bei ya mtaani, bei ya mfuko wenye vifaa hivi 12 utapatikana kwa Sh21,000 pekee.

"Wananchi wanaohitaji kutoa vifaa hivi kwa msaada kwa wananchi na vituo vya kutolea huduma za afya wafike MSD kununua, kwa wajawazito, wafike kwenye bohari zetu au maduka yetu, angalizo ni kwamba vifaa hivi viwe ni kwa ajili ya kuwapa kinamama," amesema Bwanakunu.

Seti hiyo ya vifaa vya kujifungulia mtaani inauzwa kati ya Sh55,000 hadi Sh60,000.