Maajabu ya pacha walioungana

Muktasari:

Hawakuweza kujulikana mapema hadi walipofikia umri wa kwenda shule. Hapo ndipo vyombo vya habari vilipotangaza kwa nguvu habari ya watoto wao, baada ya Mwananchi kuiibua.

        Miaka 21 iliyopita, familia ya Alfred Mwakikuti na Naomi Mshumbusi ilijaaliwa kupata watoto pacha, Maria na Consolata. Lakini hawakuwa pacha wa kawaida; walikuwa wameungana na hakukuwapo na uwezekano wa kuwatenganisha.

Hawakuweza kujulikana mapema hadi walipofikia umri wa kwenda shule. Hapo ndipo vyombo vya habari vilipotangaza kwa nguvu habari ya watoto wao, baada ya Mwananchi kuiibua.

Mwaka 2010 walimaliza elimu ya msingi na 2014 elimu ya sekondari na mwaka huu wamemaliza elimu ya juu ya sekondari.

Wakati wote huo gazeti hili limekuwa nao pamoja katika kila hatua na sasa linakuletea habari mfululizo za maisha yao kuanzia leo. Mwandishi wetu, Tumaini Msowoya anaongea nao kwa kirefu kuhusu maisha yao, changamoto, mafanikio na matamanio yao. Sasa endelea…

Tumaini Msowoya, Mwananchi [email protected]

Kilolo. Acheni Mungu aitwe Mungu kwa kuwa maajabu yake ni makubwa na hayaelezeki.

Maajabu hayo ya Mungu yanadhihirika katika muujiza wa watoto pacha, Maria na Consolata Mwakikuti waliozaliwa wakiwa wameungana.

Pacha wengi walioungana huwa wanadumu kwa kipindi kifupi na wengine hupoteza maisha yao wakati madaktari wanapojaribu kuonyesha ubingwa kwa kuwafanyia upasuaji ili watenganishwe.

Maria na Consolata ni miongoni mwa pacha ambao Mungu ameruhusu waishi pamoja mpaka leo.

Si tu kwamba, Mungu ameruhusu pacha hao kuishi, bali amekuwa akionyesha maajabu yake kwa kuwawezesha kufanikiwa katika kila hatua.

Maria na Consolata ni pacha wa kipekee waliogeuka kivutio, si tu kwa sababu wameungana, bali ni kutokana na namna walivyochukulia maisha hayo ya kuishi katika mwili mmoja na kuzishinda changamoto za kimaisha, wakifanya vizuri katika elimu ambayo ndiyo changamoto yao kubwa kwa sasa.

Hivi karibuni walihitimu kidato cha sita katika Shule ya Sekondari Udzungwa iliyopo kijiji cha Kifabaga, Kilolo mkoani Iringa.

Pacha hao walizaliwa mwaka 1996, katika hospitali ya Misheni ya Ikonda, iliyopo kijiji cha Ikonda, Wilaya ya Makete mkoani Njombe .

Mwaka 2010, walitikisa taifa baada ya kufaulu mitihani yao ya darasa la saba na hivyo kuwa na sifa ya kuendelea na masomo ya sekondari.

Miaka minne baadaye mapacha hao walitikisa tena baada ya kufaulu mitihani mingine ya kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya Maria Consolata ya Kilolo.

Hivi sasa kila mmoja ndani na nje ya nchi, anasubiri matokeo ya kidato cha sita ya kinadada hao yatakapotangazwa.

“Japo sisi ni yatima na wenye ulemavu kutokana na kuungana kwetu, haya yote si sababu ya kufeli darasani na kushindwa katika maisha. Tunajiamini na tuna uhakika kwamba tunaweza. Ni bidii tu,” anasema Consolata.

Siku niliyopata nafasi ya kushinda nao, si tu nilipata habari bali nilijifunza mengi kutoka kwao.

Ni wakarimu, wacheshi, wapole, wenye upendo na si watu wa kukurupuka kujibu, bali hutafakari kwanza.

Haichukui muda mrefu kuwazoea mapacha hawa, kwa kuwa ni wachangamfu.

Japokuwa safari yangu ya kuelekea Kidabaga, Kilolo wanakoishi mapacha hao ilikuwa ya kusuasua kutokana na uhaba wa usafiri, uchovu uliisha mara nilipobisha hodi nyumbani kwao na kupokelewa kwa nyuso zilizojaa tabasamu na bashasha.

“Karibu nyumbani kwetu, jisikie huru,” alisema mmoja wao wakati wakinikaribisha kwa furaha. Mara nyingi wanapozungumza, huwa wanatamka maneno kwa pamoja.

Pacha hawa ni watoto yatima.  Baba yao Alfred Mwakikuti na mama yao Naomi Mshumbusi walifariki dunia nyakati tofauti.

Baba alifariki wakati wakiwa na umri wa miaka mitatu na mama yao alifariki wakati wakiwa vichanga.

“Bora baba tuna kumbukumbu kidogo alikuwaje, mama yetu hatukuwahi kumuona kabisa,” anasema Consolata.

Tangu wakati huo, wamekuwa wakilelewa na wamisheni na kwa sasa wapo chini ya Shirika la Masista Wamisionari wa Shirika la Maria Consolata,  Nyota ya Asubuhi linalofanya shughuli zake Kijiji cha Kidabaga wilayani Kilolo.

Mkuu wa shirika hilo, Sister Idda Luizer anasema wanafurahi kuwalea watoto hao ambao alisema ni wacha Mungu.

Kwa kweli wamebadilika tofauti kabisa na miaka sita ya nyuma wakati nilipozungumza nao, wakiwa Ikonda wilayani Makete mara baada ya kuhitimu darasa la saba.

“Zamani tulikuwa na hisia tofauti, tulipenda tofauti lakini kwa sasa tumejikuta tukipenda na kuhisi pamoja,” anasema Consolata.

Consolata anaongea zaidi kuliko Maria na wanapotembea, hutumia mikono na miguu.

Wanao uwezo mkubwa wa kutunza kumbukumbu, kwa sababu licha ya kuwa mara ya kwanza kukutana nao ilikuwa 2010, bado waliweza kunitambua na hata kuniita kwa jina.

Mwaka huo nilipozungumza nao walitamani kusomea teknolojia ya mawasiliano, ndoto iliyozima kutokana na namna wanavyoendelea na elimu ya juu.

Ndoto yao sasa ni kuwa walimu.

Pia, wanataka kufika chuo kikuu na wakihitimu wafunge ndoa ya mume mmoja.

Namna walivyoungana  

Miujiza ya Mungu inaonekana katika umbile lao. Maria na Consolata wameungana kuanzia kifuani. Wanachangia tumbo, wana kitovu kimoja, kiuno kimoja, mikono minne yote ikiwa na nguvu za kufanya kazi na miguu mitatu.

Mguu mmoja una miguu miwili ndani yake; ni kama wameunganishwa kwa kufunikwa na ngozi.

Hii inamaanisha kwamba ukiugusa mguu huo upande mmoja wa ngozi ataitika Maria na upande mwingine, ataitika Consolata.

“Mguu huu mmoja ni wa kwetu wote, ukiugusa upande mmoja Maria anasikia na upande mwingine, mimi nasikia,” anasema Consolata.

Maumbile haya ndio sababu kubwa ya pacha hao kutembea kwa mikono na miguu.

Watembeapo mara zote Maria huwa chini kidogo na mara zote huwa anapumua kwa shida, hali inayoonyesha kwamba Consolata huwa anamuelemea mwenzake.

Matembezi yao huwa ni katika eneo la nyumbani kwao na wanapotaka kutoka, huwa wanatumia kiti cha magurudumu.

Pamoja na kwamba wameungana, kila mmoja ana sehemu zake za siri na kila mmoja anajisaidia kwa wakati wake.

Consolata anasema kila mmoja huwa anasikia maumivu kwa wakati wake.

Kitu pekee ambacho huwa wanapata maumivu kwa pamoja ni makalio ambayo huchoka zaidi wanapokaa kutokana na aina ya ulemavu. Ikiwa mmoja atahitaji kulala basi mwingine hulazimika kumvumilia mwenzake hadi anapoamka au naye aamue kulala.

“Mchana mwenzangu akisinzia, huwa tunalala tu kwenye kochi kwa sababu ni kubwa na haina haja ya kuingia chumbani. Mmoja akilala, mwingine hubaki akimsubiri mwenzake au basi wote tulale,” anasema.

Itaendelea kesho