Maalim: Hakuna atakeyezuia haki ya Wazanzibari

Maalim Seif

Muktasari:

CUF inadai mgombea wake wa urais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharrif Hamad alishinda na kunyang’anywa ushindi ambao tayari imeulalamikia katika jumuiya ya kimataifa.

Zanzibar. Zikiwa zimepita siku 215 tangu uchaguzi wa marudio ulipofanyika Zanzibar, Chama cha Wananchi (CUF), kimeendelea kulilia ushindi kinaodai kupokonywa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.

CUF inadai mgombea wake wa urais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharrif Hamad alishinda na kunyang’anywa ushindi ambao tayari imeulalamikia katika jumuiya ya kimataifa.

Akizungumza mjini hapa jana, Maalim Seif ambaye pia ni katibu mkuu wa chama hicho, alisema hakuna namna yoyote watawala wataweza kuzuia haki ya uamuzi wa Wazanzibari walioutoa Oktoba 25, 2015, lakini kinachoendelea ni njama za kuichelewesha.

Maalim aliyasema hayo wakati akitoa salamu kwa waumini wa Dini ya Kiislamu waliofika kwenye ibada ya Ijumaa katika Msikiti wa Biziredi.

“Kuna taarifa za uhakika kuhusu mbinu chafu za kuchelewesha haki ya Wazanzibari, ieleweke kwamba haki hiyo haiwezi kuzuilika tena kwa sasa,” alisema mwanasiasa huyo.

Alibainisha kwamba mojawapo wa mbinu hizo ni baadhi ya watawala kujaribu kumnyamazisha asiongee na wananchi ambao wana kiu kubwa ya kutaka kumsikiliza.

“Kuna dalili za kutaka kunikamata wanipeleke Dar es Salaam kama walivyofanya kwa masheikh, lakini nasema yote hayo ni kupoteza muda wa kuchelewesha haki ya Wazanzibari,” alisisitiza. Kiongozi huyo alisema bado anashikilia msimamo wake wa kupigania mamlaka kamili ya Zanzibar pamoja na Serikali ya Umoja wa Kitaifa visiwani humo.

Maalim Seif alidai kwamba watawala wanahaha na wanaelewa kwamba Serikali inayotawala Zanzibar haikubaliki kisheria wala kikatiba.

Alisema ipo mikakati ya kuiondoa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar iliyoanzishwa kisheria kupitia kura ya maoni na maridhiano ya kisiasa ya mwaka 2010, lakini haitawezekana.

“Nasema siyo rahisi na hao wanaojaribu hawataweza kuiondoa Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwani ni ya wananchi kupitia kura ya maoni. Hilo siyo jambo la kuchezea kama wanavyojidanganya wengine,” alisema.

Mwanasiasa huyo aliwataka watawala wasifumbe macho na kujaribu kubadilisha umiliki wa Letham Island (kisiwa cha Fungu Mbaraka), ambacho kina historia visiwani hapa na kwa mujibu wa Katiba ni sehemu ya mipaka ya nchi.

“Naelewa kwamba watawala waliopo sasa hakuna yeyote anayeweza kutetea masilahi ya Zanzibar, bali nawakumbusha kuwa hata mimi nilipokuwa Waziri Kiongozi nilikwenda katika kisiwa hicho kuweka bendera ya Zanzibar kama ishara kwamba hapo ni mali ya visiwa hivi,” alisisitiza.