Wednesday, May 16, 2018

Maalim Seif na Ramadhan

 

By Muhammed Khamis, Mwananchi mkhamis@mwaananchi.co.tz

Zanzibar. Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad amewataka wafanyabiashara Zanzibar kuutumia mfungo wa Ramadhani kujiongezea baraka na neema siyo kuongeza bei ya bidhaa.

Maalim Seif alisema wapo baadhi ya wafanyabiashara kwa sababu wanazozijua wao, wamekuwa wakiongeza bei bidhaa zao.

Alisema kwamba ni vyema wafanyabiashara kuutumia mfungo wa Ramadhan kuuza bidhaa zao kulingana na bei halisi.

Pia, aliwataka wananchi kufanya ibada na kuomba toba kwa Mwenyezi Mungu.

Baadhi ya wafanyabiashara walisema wanalazimika kuongeza bei za bidhaa kutokana na wakulima nao kupandisha.

Mfanyabiashara, Said Maulid katika soko la Mombasa Unguja, alisema kuongezeka kwa mahitaji katika kipindi cha mfungo wa Ramadhan husababisha kupanda bei kwa bidhaa.

Waumini wa Kiislam duniani hutumia mfungo wa Radhaman kuomba msamaha kwa Mwenyezi Mungu, huku wenye uwezo wakiitumia kuhudumia maskini na yatima. Baadhi ya wafanyabiashara hutumia nafasi hiyo kupandisha bei za bidhaa na kusababisha ugumu wa maisha kwa waumini. Tayari, Serikali imewaonya watakaothubutu kufanya hivyo.

-->