RIPOTI YA ALMASI, TANZANITE: Mabadiliko makubwa Baraza la Mawaziri

Rais John Magufuli akipokea taarifa ya Kamati Maalumu ya Bunge ya kuchunguza madini ya Tanzanite na almasi kutoka kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati wa hafla iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam jana. Picha na Ikulu

Muktasari:

KAULI YA MAGUFULI

  • Rais Magufuli amekabidhi taarifa hizo kwa viongozi wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama na ameagiza uchunguzi ufanyike ili wote waliohusika kusababisha upotevu mkubwa wa fedha za umma wachukuliwe hatua za kisheria haraka
  • Pia amewaagiza viongozi hao kuweka ulinzi katika maeneo yenye rasilimali za Taifa ikiwemo migodi ya Tanzanite na almasi.
  • Rais Magufuli amewataka viongozi na watendaji waliotajwa katika ripoti hizo popote walipo wakiwemo wateule wa Rais wachukue hatua za kiuwajibikaji wakati uchunguzi unaendelea kufanywa.

Dar es Salaam. Ripoti ya uchunguzi wa biashara ya almasi na Tanzanite iliyotaja mawaziri wawili, itasababisha Rais John Magufuli alazimike kufanya mabadiliko makubwa katika baraza lake la mawaziri, ikiwa ni takriban miezi 20 tangu aliunde Desemba 10, 2015.

Huku nafasi ya Profesa Sospeter Muhongo ikiwa wazi baada ya kuvuliwa uwaziri wa Nishati na Madini kutokana na sakata la makinikia, na Dk Possy Abdallah akiachia ngazi baada ya kuteuliwa kuwa balozi, Baraza la Mawaziri sasa lina nafasi nyingine mbili zilizo wazi baada ya kupoteza wajumbe wengine wawili.

Jana, George Simbachawene, alilazimika kuachia nafasi yake ya Waziri wa Tamisemi, na Edwin Ngonyani kuachia nafasi ya naibu waziri wa Nishati na Madini muda mfupi baada ya Rais Magufuli kuwataka wakae pembeni kutokana na kutajwa katika ripoti ya Kamati Maalumu ya Bunge iliyoundwa kuangalia uchimbaji, usimamizi na udhibiti wa almasi na Tanzanite.

Uamuzi huo unalifanya Baraza la Mawaziri, ambalo lilikuwa na wajumbe 32, kubakiwa na mawaziri 28.

Katika hafla ya kukabidhi ripoti hizo mbili Ikulu jijini Dar es Salaam jana, Rais Magufuli alionekana kusikitika wakati akielekea kutoa wito kwa wateule wake kukaa pembeni kupisha uchunguzi baada ya kutajwa katika ripoti ya almasi na Tanzanite.

“Kwenye taarifa hii hii ya kamati yako (Spika Job Ndugai), wako watu wametajwatajwa, na wengine mimi ndio nilihusika kuwateua,” alisema Rais na kuweka kituo kirefu.

“Sasa ukishatajwatajwa, inawezekana uko so much clean, lakini umetajwa; inawezekana wewe ni mchapakazi kweli, lakini umetajwa, inawezekana wewe ni mpole tena handsome kweli, lakini umetajwa. Na umetajwa na wabunge.”

Huku akitaja majina ya baadhi ya wajumbe, Rais alisema anaamini kuwa wajumbe wa kamati hiyo hawawezi kumuonea mtu yeyote kwa sababu wabunge wameapa kuitetea nchi.

“Sasa, kwa sababu mimi ndiye niliwateua--inawezekana wengine wako kwenye position (nafasi) fulani au niliwateua wakaenda mahali fulani, na kwa sababu hizi ripoti zote mbili za almasi na Tanzanite nilizosema nimezipokea zote--, kwanza naagiza vyombo vya ulinzi na usalama, vifuatilie yote haya na vifanye haraka,” alisema Rais Magufuli.

“Lakini la pili, wale ambao wametajwatajwa kwenye ripoti hiyo ambao ni wateule wangu; labda ni waziri, au naibu waziri, au katibu mkuu au RAS (katibu tawala wa mkoa), au DC (mkuu wa wilaya),  au mkurugenzi.

“Inawezekana ulifanya kule na sasa ni mkuu wa wilaya, lakini umetajwa kwenye ripoti hii; na ili vyombo vya usalama vifanye kazi vizuri--haviwezi kufanya vizuri na wewe uko hapo-- ni matumaini yangu (waliotajwa) watalizingatia hili. Ni matumaini yangu watakaa pembeni.”

Baada ya taarifa hiyo, Simbachawene na Ngonyani waliripotiwa kuwa wanafuatilia ripoti hiyo, lakini baadaye mchana wakatangaza kuachia ngazi.

Kuondoka kwao kunafanya mawaziri walioshindwa kwenda na kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano kufikia wanne baada ya Charles Kitwanga, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, kuwa wa kwanza kutgumbuliwa kutokana na kuingia bungeni kujibu maswali ya Serikali akiwa amekunywa pombe.

Mabadiliko madogo aliyoyafanya Rais Magufuli hayakumuacha salama Nape Nnauye aliyekuwa waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo aliyeondolewa kwa kilichodaiwa kuunda kamati ya kuchunguza tukio la uvamizi wa Clouds Media.

Nafasi ya Nape ilichukuliwa na Harrison Mwakyembe aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria huku Profesa Palamagamba Kabudi akiziba pengo hilo.

Muhongo alifuatia kutokana na kushindwa kusimamia vizuri suala la usafirishaji mchanga wa madini kwenda nje ya nchi, hiyo ikiwa ni mara ya pili mbunge huyo  wa Musoma Vijijini kuwajibika baada ya kulazimika kufanya hivyo mwaka 2014 katika sakata la escrow.

Simbachawene ametajwa katika ripoti ya Tanzanite kutokana na kuridhia mabadiliko katika mauzo ya kampuni ya uchimbaji ya Tanzanite na utoaji leseni kinyume na taratibu wakati akiwa Waziri wa Nishati na Madini, nafasi aliyoshika kwa muda mfupi mwaka 2015 baada ya Profesa Muhongo kuwajibika.

Ngonyani pia amehusishwa na sakata hilo kutokana na  kuongoza kamati maalum iliyoshauri Serikali isinunue hisa za kampuni inayoendesha mgodi wa almasi wa Williamson Diamonds Limited kwa dola 10 milioni za Kimarekani na kuikosesha Serikali mapato ya dola 300 milioni ambazo sasa zinaenda kwa kampuni ya Petra Diamond iliyoinunua.

Ripoti hizo mbili zilisomwa kwa kifupi na kuna uwezekano idadi ya wanaotakiwa kukaa pembeni kuwa kubwa zaidi ya waliotajwa na wenyeviti wa kamati hizo.

Rais pia alikabidhi ripoti hizo kwa Takukuru akitaka ifanye uchunguzi zaidi kabla kuchukua hatua.

“Wale waliokaa miaka 20 lazima washughulikiwe na nitashangaa nikiwaona hadi leo bado hawajashikwa,” alisema Rais.

Kamati hizo zimebaini dosari mbalimbali katika usimamizi wa mapato ya serikali, udhibiti wa rasilimali, udhaifu katika mikataba, udhaifu wa mifumo, sheria mbovu na kutowajibika ipasavyo kwa watu waliopewa dhamana ya kusimamia rasilimali za nchi.

Wengine wanaotakiwa kukaa pembeni ni Eliakim Maswi, ambaye alikuwa katibu mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini. Maswi alisusa kufanya ziara mgodini baada ya kukuta kile alichokiita madudu na hivyo kutosimamia vyema rasilimali za nchi.

Wakati ripoti ya almasi ilimtaja aliyekuwa mwenyekiti wa kamati iliyochunguza mchanga wa makinikia, Profesa Abdulkarim Mruma kuwa alisaini madeni ambayo mwekezaji aliibambikia Serikali, Rais Magufuli alimtetetea jana kuwa alimtuma huko kwa kazi maalumu.

Watendaji wengine ni katibu mkuu wa nishati na madini, James Mdoe.

Rais Magufuli pia alimshauri Spika Ndugai kuangalia uwezekano wa kubadilisha kanuni ili wabunge wanaotajwatajwa waweze kushughulikiwa na Bunge, au kuviandikia vyama vyao ili vichukue hatua.

Alisema iwapo Bunge litaviandikia vyama, CCM itawaonya, kuwajadili na kuwapa nafasi ya kujitetea au kuchukua hatua nyingine.

Wabunge wa CCM waliotajwa katika ripoti hiyo na ambao hawana nafasi Serikalini kwa sasa ni William Ngeleja, ambaye alitajwa sakata la escrow, makinikia na sasa Tanzanite, na Profesa Muhongo.

Waziri Mkuu

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema wakati akipokea ripoti hizo alikuwa na uwezo wa kufanya maamuzi kama mtendaji mkuu wa Serikali, lakini hakufanya hivyo kwa ajili ya kumpa nafasi muasisi wa vita hiyo, Rais Magufuli.

Alisema imefika wakati rasilimali za nchi ikiwamo madini zikatumika kunufaisha Watanzania, lakini suala hilo halitafanikiwa bila kuwa na uzalendo.

“Serikali ipo pamoja na wabunge,na ipo tayari kupokea ushauri na kuufanyia kazi kwa maslahi ya taifa,”alisema.

Naye Spika wa Bunge, Job Ndugai alisema kutokana na mapendekezo ya kamati hizo ya kutaka kubadili sheria na kupitia mikataba ya madini, Bunge hilo lipo tayari kufanya kazi kwa manufaa ya Taifa.

Alisema, Shirika la Madini la Taifa (Stamico) limeonyesha udhaifu mkubwa kwa kushindwa kusimamia makubaliano ya kimkataba na mashirika ya madini ya kigeni hali iliyosababisha kupata hasara.

Pia, alitaka bodi za madini nchini kuboresha utendaji kazi kwa kutembelea maeneo husika ili kubaini kasoro zinazojitokeza kuliko kusubiri vikao.

“Kama kamati zangu zimeweza kuona mambo yote hayo kwa mwezi mmoja, unakaa kwenye kamati miaka mitatu na hujui kitu? Hii ni aibu,” alisema Ndugai.