Mabadiliko yafanyika matumizi ya ARV

Muktasari:

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema jana kuwa matumizi ya ARV mapema baada ya kugundulika kuwa na VVU  yatasaidia kudhibiti maambukizi mapya.

Dar es Salaam. Kuanzia mwakani watu wote watakaobainika kuwa na Virusi Vya Ukimwi (VVU) wataanza kutumia dawa za kufubaza makali (ARV) bila kujali kiwango chao cha kinga ya mwili (CD4).

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema jana kuwa matumizi ya ARV mapema baada ya kugundulika kuwa na VVU  yatasaidia kudhibiti maambukizi mapya.

Uamuzi huo alisema unatokana na mwongozo uliotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO) Septemba mwaka jana kuwa wanachama wake wahakikishe wanaobainika kuwa na VVU wanaanza dawa mara moja. Awali, walikuwa wanaanza kutumia dawa baada ya kiwango cha CD4 kushuka hadi kufikia 350 au 300 na kwa kawaida binadamu akiwa mzima wa afya ana CD4 600.