Mabaraza kata kusimamiwa na mahakimu

Jaji Mkuu, Prof Ibrahim Juma (kushoto) akisalimiana na watumishi wa Mahakama ya Wilaya ya Nzega alipowasili kukagua shughuli za Mahakama. Jaji Mkuu ameanza ziara ya kikazi katika mkoa wa Tabora na Kigoma ambayo ni Kanda ya Tabora. Na Mpigapicha Maalum

Muktasari:

        Hali hiyo inaelezwa itasaidi kupunguza kesi zinazofunguliwa katika mahakama za mwanzo

Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma amewataka mahakimu wa mahakama za mwanzo nchini kusimamia mabaraza ya kata yaliyoanzishwa kwa Sheria ya Mwaka 1985.

Alisema mabaraza hayo ni sehemu muhimu katika mfumo wa utoaji haki, kutokana na kazi yake ya kusuluhisha na kupatanisha mashauri madogo madogo ya jinai na madai.

Jaji Mkuu alisema mfumo wa utoaji haki kupitia mabaraza ya kata unawaunganisha wananchi tofauti na pale kesi inaposikilizwa mahakamani, ambako mara zote aliyeshindwa hujenga uadui na aliyeshinda.

Profesa Juma aliyasema hayo juzi wakati akizungumza na watumishi wa mahakama mkoani Tabora, akiwa kwenye ziara ya mkoa huo na Kigoma.

Alisema iwapo mabaraza ya kata yatasimamiwa ipasavyo ni wazi idadi ya kesi zinazofunguliwa kwenye mahakama za mwanzo nchini itapungua kwa kiwango kikubwa kwa kuwa kesi nyingi zitaamuliwa kwenye mabaraza hayo kwa njia ya usuluhishi na upatanishi.

Aliongeza kuwa kesi zote zinazosajiliwa nchini, asilimia 74 ni za mahakama za mwanzo.

Profesa Juma alisema ili kuimarisha mfumo wa utoaji haki kupitia mabaraza ya kata, Mahakama ya Tanzania imeandaa mpango wa mafunzo utakaowakutanisha mahakimu na wajumbe wa mabaraza ya kata.

Pia Profesa Juma aliwataka watumishi wa mahakama kuzingatia maadili ya kazi na kutoa haki kwa wakati, kwa kuwa kufanya hivyo watachangia katika kukuza uchumi wa Taifa.

Alisema mashauri yanapomalizika kwa wakati hutoa nafasi kwa wananchi kufanya shughuli za uzalishaji, hivyo kukuza uchumi.

“Mnapofanya kazi ya utoaji haki mjisikie ni sehemu ya kujenga uchumi maana bila ya haki hakuna amani”, alisema Profesa Juma.

Alisema Mahakama ina mchango mkubwa katika kudumisha amani, utulivu na umoja ambayo ni sehemu ya Dira ya Taifa ya mwaka 2025.

Kuhusu matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) ndani ya Mahakama, Jaji Mkuu alisema tayari Mahakama imeanza kutumia mfumo huo kwa kukusanya takwimu za mashauri kuanzia ngazi ya mahakama za wilaya.

Pia, alisema baadhi ya majengo ya mahakama tayari yanatumia Tehama huku akitolea mfano jengo la Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya na Kituo cha Mafunzo Kisutu.

Aliwataka watumishi wa Mahakama wa kada zote kujiendeleza hasa katika matumizi ya Tehama ili mahakama itekeleze wajibu wake wa kutoa haki kwa wakati.

Alisema kupitia Tehama mahakama itatoa haki kwa haraka na kwa wakakti hivyo wananchi wataongeza imani yao kwa mhimili huo.

Jaji Mkuu alitembelea mahakama za mwanzo wilaya za Nzega, Igunga.Tabora na Kigoma zinaudwa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora.