Jinsi ukaguzi wa basi ulivyookoa maisha ya abiria walikuwa wakisafiri jana Jumanne

Muktasari:

  • Kila ifikapo Desemba, idadi ya abiria wanaosafiri kwenda mikoani kusherekea sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya huwa kubwa kulinganisha na mabasi yanayotoa huduma hiyo hivyo kusababisha msongamano.

Mabasi 20 kati ya 400 yaliyokuwa yakisafirisha abiria kwenda mikoani, yamezuiwa na askari wa usalama barabarani Kituo cha Mabasi Ubungo (UBT) kuendelea na safari huku manne kati ya hayo yakisitishwa kutoa huduma ya usafiri kutokana na ubovu.

Kila ifikapo Desemba, idadi ya abiria wanaosafiri kwenda mikoani kusherekea sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya huwa kubwa kulinganisha na mabasi yanayotoa huduma hiyo hivyo kusababisha msongamano.

Baadhi ya wamiliki wamekuwa wakitumia uhaba huo kutoa mabasi hata yale ambayo ni mabovu ili kubeba abiria jambo linaloelezwa kuwa chanzo cha ongezeko la ajali kila ifikapo mwishoni mwa mwaka.

Kutokana na hali hiyo, kikosi cha usalama barabarani UBT jana kilifanya ukaguzi na kubaini kuwa mabasi 20 hayakuwa na sifa ya kubeba abiria.

Mkuu wa usalama barabarani UBT, Inspekta Samwix Ibrahimu aliongoza ukaguzi huo wa injini, breki, upepo, ubora wa tairi na vifaa mbalimbali.

Katika ukaguzi huo Basi la Shambalai lililokuwa likielekea Tanga lilibainika kuwa na tatizo katika mfumo wa usukani. Baada ya dereva wa basi hilo kuambiwa azungushe usukani kuelekea upande wa kushoto, chuma kinachoushikilia kikakatika hali iliyomstua Inspekta Ibrahimu na kusema “Gari hili lilikuwa linaenda kuanguka.” Baada ya kumshukuru Mungu kwa kupiga ishara ya msalaba, aliwataka abiria washuke ndani ya basi.

Akizungumza baada ya ukaguzi huo Inspekta Ibrahimu alisema, “Tumejipanga hakuna basi bovu litakalopita hapa. Tunataka kusiwepo ajali mwisho wa mwaka kama ilivyozoeleka kwamba kila mwisho wa mwaka ajali zinakuwa nyingi. Nadhani umeona mwenyewe Basi la Shambalai tumelikagua na kukuta ni bovu, kama tungeruhusu lipite basi lingeanguka njiani.”

Hata hivyo, mmiliki na dereva wa basi la Shambalai Express, Idrisa Ayoub alisema magari yao wanayakagua vizuri na kilichotokea jana hajawahi kukiona kwani chuma hicho huwa hakikatiki, bali kinachomoka.

“Wakati wanakagua waliniambia nikate kushoto, chuma hicho kikakatika. Hata wao wameshangaa, maana si rahisi kukatika lakini bado tunachunguza ili kujua nini chanzo,” alisema.

Aliwashukuru wakaguzi hao kwa kusaidia kuokoa maisha yake na abiria na kwamba tukio hilo liko kiufundi zaidi.

“Tumependa wanachofanya kwa kweli. Japo tutachelewa kufika lakini wametuokoa,” alisema mmoja wa abiria, Hamis Juma ambaye pamoja na wenzake, waliokuwa katika basi hilo walirudishiwa nauli zao.