Mabeyo: Tutatumia siku mbili kukinyanyua kivuko cha MV Nyerere

Muktasari:

Kivuko cha Mv Nyerere kitapinduliwa chini juu hapo kilipo badala ya kuvutwa hadi mwaloni kama ilivyotangazwa hapo awali

Dar es Salaam. Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Jenerali Venance Mabeyo amesema kivuko cha Mv Nyerere kitapinduliwa chini juu hapo kilipo badala ya kuvutwa hadi mwaloni kama mipango ya awali ilivyokuwa.

Jenerali Mabeyo ametoa kauli hiyo leo, Septemba 23, 2018 eneo la Ukara wilayani Ukerewe mkoani Mwanza baada ya kuwasili kifaa maalumu kitakachotumika kukipindua kivuko kilichozama Septemba 20,2018 na kusababisha vifo vya watu 224 hadi sasa.

“Tuombeni tufanikiwe na tutafanikiwa. Tunaamini kazi hii ya kukipindua kivuko hiki itaweza kuchukua siku mbili au tatu,” amesema Jenerali Mabeyo

“Kivuko hiki kimejikita chini na kifaa hiki kitaingiza upepo utakaoingia kwenye maboya yatakayosaidia kukipindua na hatua ya kukipindua itasaidia kivuko hiki kutoharibika,” ameongeza

Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe amesema shughuli ya uokoaji inafanywa na Watanzania wenyewe na si watu kutoka nje.

Pia, amewapiga marufuku watendaji wa taasisi zilizopo chini ya wizara hiyo kukodi vifaa kwa ajili ya shughuli hiyo na kwamba kazi hiyo ipo chini ya uratibu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ).

Mbali na hilo, Mhandisi Kamwelwe amesema bado watu wanaendelea kuchangia waathirika wa kivuko hicho na tayari Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), imekabidhi mchango wa Sh50milioni.

“Hatua ya SMZ kutoa kiasi hicho, inafikisha jumla ya Sh240 milioni  zilizochangwa mpaka sasa,” amesema Mhandisi Kamwelwe ambaye pia ni Mbunge wa Katavi.