Mabingwa wa upasuaji Marekani kuwapa mafunzo madaktari Moi

Muktasari:

Wakufunzi hao watafanya mafuno hayo na kutoa huduma kwa wagonjwa kwa muda wa wiki mbili.


Dar es Salaam. Wakufunzi kutoka Chuo Kikuu cha Colorado, Denver cha Marekani watawapa mafunzo madaktari wa Taasisi ya mifupa (MOI) ili kuwapa za uchunguzi, matibabu na upasuaji.

Wakufunzi hao watafanya mafuno hayo na kutoa huduma kwa wagonjwa kwa muda wa wiki mbili.

Akizungumza leo Juni 13, 2018 Mkurugenzi wa Moi Dk Respecious Boniface amesema kuwa mafunzo yanayotolewa yanahusu matumizi ya mashine ya Ultra Sound wakati wa upasuaji wa ubongo na mgongo.

Amesema pia, wakufunzi hao watafundisha njia za kutumia darubini maalumu na ya kisasa (Neuromicroscope) inayotumika kwenye upasuaji wa kibingwa wa matundu wa mgongo, mishipa ya fahamu na ubongo.

"Mafunzo haya yatakwenda sambamba na upasuaji  wa ubongo , mgongo na mishipa ya fahamu ikiwa ni sehemu ya mafunzo kwa vitendo," amesema Dk Boniface.

Daktari bingwa wa upasuaji ,  Nicephorus Rutabasibwa amesema pamoja na mambo mengine wakufunzi hao wamekuja na msaada wa vifaa tiba vya kisasa vya upasuaji wa ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu vyenye thamani ya zaidi ya Sh18 milioni.

“Vifaa hivi vitakabidhiwa Moi ili viendelee kutumika baada ya mafunzo," amesema Dk Rutabasibwa