Mabomu yatumika kuwatawanya madiwani

Mwananchi akiingizwa kwenye gari ya polisi baada ya kukamatwa kwenye tukio la madiwani kufunga barabara.Picha na Rehema Matowo

Muktasari:

  • Madiwani wamefunga barabara kushinikiza GGM kulipwa ushuru wa huduma.

Geita. Polisi wametumia mabomu ya machozi kuwatawanya wananchi na madiwani waliofunga  barabara ya kuingia kwenye Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM).

Katika tukio hilo leo Alhamisi asubuhi, madiwani wawili na baadhi ya wananchi wamekamatwa na polisi.

Kabla ya kutumia mabomu, polisi walitoa onyo wakiwataka wananchi na madiwani hao kutawanyika kwa amani lakini waligoma.

Madiwani wa  halmashauri mbili za Wilaya ya Geita jana Jumatano walitanga mgogoro na GGM wakishinikiza kulipwa Dola 12 milioni za Marekani zinazotokana na ushuru wa huduma kuanzia mwaka 2004 hadi 2013.

Walitangaza kuzuia magari ya mgodi kwa    kufunga barabara  na pia kufunga maji yanayoingia mgodini kutoka Ziwa Victoria.

GGM iliwatangazia wafanyakazi wake jana kutofika kazini leo kutokana na mgogoro huo.

Polisi hivi sasa wameimarisha ulinzi kwenye maeneo ya Nungwe uliko mradi wa kusambaza maji mgodini, eneo la uwanja wa ndege na geti la kuingia mgodini.

Mkuu wa Wilaya ya Geita, Herman Kapufi na mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Musukuma wameingia mgodini baada ya madiwani na wananchi kutawanywa.