Machungu, matamu ya mwaka 2017

Muktasari:

Ni mwaka ulioshuhudia mapinduzi ya kimfumo hususan katika sekta ya madini baada ya Serikali kukunjua makucha kuhakikisha rasilimali hiyo ya Taifa inawanufaisha wananchi.

Wiki mbili zimebaki kuufunga mwaka 2017 na kuingia 2018. Kama ilivyokuwa kwa miaka mingine, 2017 umekuwa na milima na mabonde mengi, mambo kadha wa kadha yamejitokeza, ya simanzi na furaha.

Ni mwaka ulioshuhudia mapinduzi ya kimfumo hususan katika sekta ya madini baada ya Serikali kukunjua makucha kuhakikisha rasilimali hiyo ya Taifa inawanufaisha wananchi.

Pia ni mwaka uliogubikwa matukio lukuki yaliyobeba sura ya kitaifa na kimataifa.

Baadhi ya matukio yaliyotikisa ni sakata la mchanga wa madini ya dhahabu (makinikia), kushambuliwa kwa risasi Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, ajali ya wanafunzi wa Shule ya Lucky Vincent, mauaji katika wilaya za Kibiti na Rufiji, vigogo kufikishwa mahakamani, utekaji na shubiri iliyovipata vyombo vya habari.  

Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (CKD), Dk Richard Mbunda anasema baadhi ya matukio yanaonyesha jinsi gani vyombo vya ulinzi na usalama vimeshindwa kutimiza wajibu wake.

“Kuishi kwa woga, kuhofia kutekwa, atashambuliwa au atauawa, ilikuwa huko nyuma ili sasa imerudi. watu wanatekwa,” alisema Dk Mbunda.

Makinikia

Baada ya Rais John Magufuli kuunda tume mbili kuchunguza madai ya wizi na ufisadi unaodaiwa kufanywa na wawekezaji kwa zaidi ya miaka 19 iliyopita tangu walipoanza uzalishaji wa dhahabu, ilibainika kuwapo kwa kasoro kadhaa zilizolisababishia Taifa kukosa mapato.

Ripoti hizo ndizo zilizozaa mazungumzo kati ya Serikali ya Tanzania na Kampuni ya Barrick Gold Corporation kuhusu kasoro zilizobainishwa na majadiliano yao yamekuwa yakielezwa na kiongozi wa timu ya Tanzania, Profesa Palamagamba Kabudi yanakwenda vyema na nchi itegemee kunufaika.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo Bisimba alizungumzia suala la makinikia akisema, “Ni suala zuri. Haki zetu za uchumi tulizopaswa kupata tunatakiwa tuzipate, lakini ninachojiuliza mwisho wa mazungumzo utakuwaje?”

Ripoti ya kamati ya kwanza iliyoongozwa na Profesa Abdulkarim Mruma ilibaini kasoro za usimamizi na Rais Magufuli alimng’oa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo katika wadhifa huo na kuivunja Bodi ya Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA).

Pia, Rais Magufuli alimsimamisha kazi mkurugenzi mtendaji wake, Dominick Rwekaza na kuagiza vyombo vya dola kufanya uchunguzi dhidi yao ikiwamo watumishi wote wa TMAA na wakibainika hatua kali zichukuliwe.

Ripoti ya pili ya kamati maalumu chini ya Mwenyekiti  Profesa Nehemiah Ossoro nayo ilibaini kuwa usafirishaji mchanga umelipotezea Taifa kati ya Sh132 trilioni na 380 tangu mwaka 1998.

Upotevu huo ulitokana na sababu mbalimbali ikiwamo ukwepaji kodi, utoaji taarifa za uongo za usafirishaji makinikia na uwajibikaji usiozingatia masilahi ya Taifa.

Aidha, ripoti hiyo ilibaini ubovu wa Sheria ya Madini na matumizi mabaya ya madaraka yaliyofanywa na mawaziri, makamishna na wanasheria katika kuingia mikataba na kutoa leseni ambazo Rais Magufuli tayari alikwishatoa zuio.

Baadhi ya majina ya vigogo waliodaiwa kuhusika na  kuisababisha Serikali hasara ni pamoja na waliokuwa wanasheria wakuu wa Serikali, Andrew Chenge na Johnson Mwanyika. Manaibu wanasheria wakuu, Felix Mrema na Sazi Salula na wakuu wa idara, mikataba Maria Ndossi Kejo na Julius Malaba.

Wengine waliotajwa; Waliowahi kuwa mawaziri wa Nishati na Madini kwa nyakati tofauti, William Ngejela, Profesa Muhongo, Daniel Yona na Nazir Karamagi.

Pia wamo, makamishna wa madini, Paulo Masanja, Dk Dalaly Kafumu na Kaimu Kamishna Ally Samaje na wote hao, Rais Magufuli aliviagiza vyombo vya dola kuwachunguza na wakibainika hatua zaidi zichukuliwe dhidi yao.

Kutokana na matatizo hayo, Serikali ilipeleka bungeni miswada mitatu ya mabadiliko ya sheria zinazohusu sekta ya madini na rasilimali inayotoa fursa mbalimbali za Taifa kunufaika.

Mbali na makinikia, Bunge pia liliunda kamati mbili zilizochunguza biashara ya madini ya Tanzanite na almasi na mara baada ya ripoti zake kukabidhiwa kwa Spika wa Bunge, Job Ndugai kisha kuzifikisha kwa Rais Magufuli vigogo kadhaa waliotuhumiwa walienguliwa.
Waliong’oka katika kashfa hiyo ni aliyekuwa Waziri Ofisi ya Rais (Tamisemi), George Simbachawene, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Edwin Ngonyani na Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara, Eliakimu Maswi.

Mauaji Kibiti

Matukio ya mauaji  katika wilaya za Kibiti, Rufiji na Mkuranga mkoani Pwani hayakuuacha mwaka huu salama, yalishtua wakazi wa maeneo hayo hususan Kibiti na kuzua mijadala na hofu kwa wakazi wa ndani na nje ya eneo hilo.

Tangu kuanza kuripotiwa kwa mauaji hayo, Januari 2015, idadi ya viongozi na wananchi waliouawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana ni zaidi ya 40, wakiwamo askari 13 wa Jeshi la Polisi huku matukio mengi yakijitokeza mwaka huu hususan kati ya Januari na Julai.

Katikati ya matukio hayo, Mei 28, Rais Magufuli alifanya mabadiliko ya Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) kwa kumteua aliyekuwa Kamishna wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro kuwa IGP kuvaa viatu vya Ernest Mangu.

Wakati Rais Magufuli akieleza kwamba atampangia kazi nyingine Mangu ambaye hivi karibuni alimteua kuwa Balozi akisubiri kupangiwa kituo cha kazi, alimtaka IGP Sirro kukomesha matukio ya kihalifu yaliyokuwa yakiendelea Kibiti.

Kuhusu matukio hayo, Dk Mbunda alisema, “Hatuhitaji kuyaona mwaka 2018 na kinachopaswa kufanywa ni kila mtu kutumia jukwaa lake iwe la kisiasa, vyombo vya habari na viongozi wa dini kukemea.”

Tundu Lissu

Septemba 7 itakuwa siku ya kukumbukwa Lissu, rais huyo wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) alishambuliwa kwa zaidi ya risasi 30 saa saba mchana akiwa katika gari nje ya makazi yake Area D mjini Dodoma muda mfupi baada ya kufika hapo akitoka kuhudhuria mkutano wa Bunge.

Taarifa za kushambuliwa kwake ziliwashtua watu wengi ndani na nje ya Tanzania, kila mmoja akisema lake. Mara baada ya taarifa hizo kusambaa, mamia ya wakazi wa Dodoma walimiminika katika Hospitali ya Mkoa alikopelekwa kwa matibabu ya awali kabla ya usiku huohuo kuhamishiwa Hospitali ya Nairobi, Kenya.

Katika mahojiano na gazeti hili hospitalini hapo hivi karibuni, Lissu alilielezea tukio hilo akisema, “Katika kipindi cha maisha yangu, hiki ni kipindi kigumu ambacho sikuwahi kukutana nacho, kinanipa mafunzo lakini hakinirudishi nyuma katika harakati za kutetea wanyonge.”

Alisisitiza kuwa tukio la kushambuliwa kwake ni la kisiasa.

Utekaji

Matukio ambayo yamekuwa yakizua mijadala mipana mwaka huu ni haya ya utekaji watu unaofanywa na watu wasiojulikana. Tukio la hivi karibuni la kutekwa na watu wasiojulikana limemfika mwandishi wa kujitegemea wa Kampuni ya Mwananchi Communicatios Limited (MCL), Azory Gwanda ambaye tangu Novemba 21 na mpaka sasa hajulikani alipo.

Azory ambaye anaripoti kutoka Kibiti na Rufiji mkoani Pwani ni miongoni mwa wananchi waliotekwa katika eneo hilo na mpaka sasa si yeye au hao wengine waliopatikana au taarifa zao kujulikana huku vyombo vya ulinzi na usalama vikieleza kuwa vinaendelea na uchunguzi.

Si Azory na watu hao wa Pwani pekee ambao wamekutana na mkasa huo, Aprili 6 wasanii wa muziki wa Hip Hop, Ibrahim Mussa maarufu ‘Roma Mkatoliki’ Monii Central Zone, Bin Laden na Imma, mfanyakazi wa  mama mzazi wa mmiliki wa Studio za Tongwe Records iliyopo Masaki Dar es Salaam, J Murder walijikuta mikononi mwa watekaji.

Iliwachukua siku mbili wasanii hao kukaa kusikojulikana hadi April 8 walipopatikana lakini Roma ambaye hakueleza kinaga ubaga ni kina nani waliowateka akisema anaviachia vyombo vya ulinzi na usalama kufanya uchunguzi lakini mpaka sasa hakuna taarifa zozote za tukio hilo.

Akizungumzia matukio hayo, Dk Bisimba alisema mauaji na utekaji yaliyokuwa yakitokea enzi za utawala wa hayati Mwalimu Julius Nyerere, kiongozi huyo alikuwa akijitokeza kuzungumzia na kukemea.

“Mlinzi mkuu wa wananchi na mali zake ni Rais, matukio kama haya hatujaona akijitokeza kuyazungumzia na kuyakemea, yeye ndiye mwenye jukumu hili kwa hiyo ili mwaka 2018 yasijitokeze Rais asimame katika hili,” alisema.

Uvamizi wa Clouds

Haikuwahi kutokea tangu nchi ipate Uhuru pale Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda akiwa na askari watano wenye silaha za moto, usiku wa saa nne, Machi 17 alipodaiwa kuvamia kituo cha Redio na Televisheni cha Clouds Media Group (CMG).

Ilidaiwa kuwa lengo la Makonda lilikuwa kuwashinikiza watangazaji wa kipindi cha ‘Shilawadu’ warushe video ya kumchafua Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima.

Tukio hilo lilimwingiza katika ugomvi mkubwa na wadau wa habari ambao walimtangaza kuwa adui wa tasnia ya habari pamoja na kumfungia kuripoti habari zake zuio ambalo lilidumu kwa zaidi ya miezi mitatu kabla ya kuondolewa pasi na kuomba radhi kama alivyopaswa.

Tukio hilo lilimfanya aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye kuunda kamati ya kuchunguza kitendo hicho lakini siku moja baada ya kukabidhiwa ripoti ya uchunguzi, Rais Magufuli alitengua uteuzi wake, Machi 23 na nafasi yake kuchukuliwa na Dk Harrison Mwakyembe.

Ajali ya wanafunzi Lucky Vincent

Mei 6 ilikuwa siku ya simanzi na majonzi makubwa baada ya taarifa ya ajali mbaya ya basi lililokuwa limewabeba wanafunzi wa Shule ya Lucky Vincent ya jijini Arusha waliokuwa wakienda kufanya mtihani wa ujirani mwema katika Shule ya Tumaini English Medium Junior.

Ajali hiyo ilitokea baada ya basi hilo kutumbukia katika Mto Marera ulioko Mlima Rhotia, Karatu mkoani Arusha na kusababisha vifo 35 kati yake wanafunzi 32, walimu wawili na dereva mmoja huku wanafunzi watatu pekee; Doreen (13), Sadia (12) na Wilson (12), wakisalimika.

Aliyekuwa Mbunge wa Singida Kaskazini (CCM), Lazaro Nyalandu aliratibu safari ya watoto hao walionusurika kwenda kupata matibabu zaidi katika Hospitali ya Mercy iliyopo Sioux City, Lowa nchini Marekeni kwa msaada wa Shirika la Siouxland Tanzania Educational Medical Ministries (STEMM).

Majeruhi hao waliondoka nchini Mei 15 kwa ndege maalumu ya Shirika la Samaritan’s Purse inayosimamiwa na mtoto wa mwinjilisti mkubwa wa Marekani, Franklin Graham ambayo pia iliwarejesha nchini Agosti 18.

Katika kuwaenzi waliofariki kwenye ajali hiyo, Bodi ya Wadhamini STEMM ilitangaza kuwasomesha watoto hao watatu hadi elimu ya Chuo Kikuu chochote duniani.

Kesi za vigogo

2017, pia umekuwa mwaka ulioshuhudia vyombo vya dola vikiwafikisha mahakamani vigogo mbalimbali kujibu tuhuma zinazowakabili na wengine mpaka sasa bado wapo korokoroni kutokana na kesi zao kutokuwa na dhamana.

Juni 19, sakata la ufisasi wa mabilioni ya akaunti ya Tegeta Escrow lilichukua sura mpya baada ya Mkurugenzi wa Kampuni ya VIP Engeneering & Marketing ambaye pia alikuwa Mkurugenzi mwenza wa kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Ltd (IPTL), James Rugemalira na mmiliki wa kampuni ya PAP, Habirnder Seth Singh  walifikishwa mahakamani na Takukuru na kusomewa mashtaka kadhaa likiwamo la uhujumu uchumi. Kesi hiyo inaendelea na watuhumiwa wako rumande.

Viongozi wa michezo hawakuachwa salama na Takukuru baada ya aliyekuwa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi, Katibu Mkuu wake, Celestine Mwesigwa na mhasibu Nsiande Mwanga, Rais wa Klabu ya Simba, Evance Aveva na makamu wake, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ pia walifikishwa na mahakamani na moja ya makosa wanayokabiliwa nayo ni la uhujumu uchumi.

Februari haikumwacha salama mfanyabiashara maarufu, Yusuf Manji alipofikishwa mahakamani akituhumiwa kutuma dawa za kulevya kisha akawa na kesi nyingine ya uhujumu uchumi iliyomweka rumande kwa zaidi ya mwezi mmoja kisha kesi hiyo kufutwa na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).

Vyombo kufungiwa

Mwaka huu unakwenda kumalizika huku ikishuhudiwa vyombo vya habari hususan magazeti yakifungiwa kwa vipindi tofauti. Magazeti yaliyofungiwa ndani ya mwaka huu ni MwanaHalisi, Mawio, Raia Tanzania na Tanzania Daima.

Dawa za kulevya

Februari, vita ya watumiaji na wauzaji wa dawa za kulevya ilichukua sura mpya baada ya  Makonda kutangaza hadharani majina ya watu aliodai kuwa wanajihusisha kwa namna moja au nyingine na biashara hiyo.

Baadhi ya majina aliyoyataja na kuwataka kuripoti Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam ni Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Manji, Askofu Gwajima na mbunge wa zamani wa Kinondoni (CCM), Idd Azzah.

Vifo vya vigogo

Tunaufunga mwaka tukiwa tumeagana na baadhi ya viongozi wa Taifa ambao wamehitimisha safari yao hapa duniani. Baadhi yao ni aliyekuwa mbunge wa Songea Mjini, (CCM) Leonidas Gama, mkuu wa mikoa na waziri wa zamani, Joel Bendera aliyefariki Desemba 6 na mbunge wa zamani wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo, George Kahama.

Pia, tasnia ya habari imeshuhudia vifo vya wapendwa wake, Muhingo Rweyemamu, Rose Athuman, Abdallah Yakuti na Joyce Mmasi ambao kwa nyakati tofauti waliwahi kufanya kazi MCL.

Mbali ya hao wengine waliopoteza maisha ni John Kulekana na Muganyizi Mutta.