Madaktari 14 MNH wapelekwa Hospitali ya Rufaa Musoma

Muktasari:

  • Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imeanza programu ya kupeleka madaktari wake katika hospitali za rufaa za mikoa yote nchini.

Dar es Salaam. Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imepeleka madaktari 14 katika Hospitali ya Rufaa Musoma mkoani Mara kwenda kutoa huduma za upasuaji wa pua, masikio, macho na koo.

Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Huduma kwa Wateja MNH, Aminael Aligaesha alisema jana kuwa hospitali hiyo imeanzisha programu endelevu ya Mkoba ambayo kila robo ya mwaka itakuwa inapeleka madaktari bingwa katika hospitali zote za rufaa nchini.

“Hii ni programu endelevu itakayokuwa inafanya kazi ya kutembelea hospitali nne kila baada ya robo mwaka na kwa mara ya kwanza jana (juzi) tumepeleka wataalamu 14 Musoma na watafanya kazi kwa siku tano,” alisema Aligaesha

“Lengo la kuanzisha huduma hii ni kutaka kupunguza wingi wa wagonjwa ambao wanaletwa Muhimbili kupata huduma kubwa ikiwamo upasuaji, lakini pia kubadilishana uzoefu na wataalamu waliopo katika hospitali za rufaa mikoani na wa hapa Muhimbili.”

Alisema pia hospitali hiyo inataka kuwapa uwezo madaktari bingwa walioko katika hospitali hizo za rufaa mikoani kufanya upasuaji ili kupunguza gharama kwa wagonjwa kusafiri kutoka mikoani kufuata huduma kubwa Muhimbili.

“Programu hii ni sehemu ya mpango mkakati wa hospitali iliyojihakikishia inatembelea hospitali za rufaa za mikoa yote nchini ili kushirikiana nao katika kutoa huduma kwa wananchi ambao wangepewa rufaa kuja Muhimbili kupata matibabu,”alisema.

Pia, aliongeza kuwa madaktari hao kutoka Muhimbili watakuwa na kazi ya kuwajengea uwezo wataalamu wa hospitali za rufaa za mikoani katika huduma za upasuaji wa pua, koo, macho na masikio.