Madaktari walivyomsaidia mrembo kutoa uhai wake

Muktasari:

  • Kifo chake kimeidhinishwa na Serikali ya Uholanzi kwa mujibu wa sheria

Paris, Uholanzi. Wahenga walisema kuwa uyaone! Kila kukicha kuna vituko vya hapa na pale duniani. Nchini Uholanzi kuna mrembo mmoja ambaye kwa ridhaa yake ameamua kunywa sumu aliyopewa na daktari kisha akalala akisubiri kifo chake.

Kifo cha mrembo huyu kiliidhinishwa na Serikali ya Uholanzi. Lakini Aurelia Brouwers hakuwa katika hali mbaya ya ugonjwa aliruhusiwa kukatisha maisha yake kutokana na maradhi ya akili.

‘’Nina miaka 29 na nimechagua kujitolea kutolewa uhai. Nimechagua kifo kwa sababu nina matatizo ya afya ya akili. Ninateseka sana bila matumaini. Kila pumzi nayovuta ni mateso.’’

Runinga ya RTL nchini humo ilitumia wiki mbili ikimrekodi Aurelia akiwa anakaribia siku zake za kuondoka duniani-alifariki saa nane mchana Ijumaa, Januari 26 mwaka huu.

Kwenye ubao mweupe nyumbani kwake alizungushia alama ya wino mzito mweusi siku zilipokuwa zikisogea kuelekea kifo chake.

Kwa mujibu wa shirika la Habari la BBC, katika kipindi cha wiki mbili za mwisho, alitumia muda wake na wapendwa wake, pia alitembelea eneo ambalo alilichagua kufanyika shughuli za mazishi.

Kukatisha uhai kutokana na maumivu au maradhi yasiyotibika ni kinyume cha sheria katika nchi nyingi, lakini nchini Uholanzi inaruhusiwa kama daktari atajiridhisha kuwa mgonjwa anateseka sana kukiwa hakuna matarajio ya kupata nafuu na kama hakuna njia mbadala kwa ajili ya kumpatia nafuu mgonjwa.

Watu 6,585 walikatishwa uhai Uholanzi mwaka 2017 miongoni mwao 83 kutokana na maradhi ya akili.

Alichokisema

“Sijawahi kuwa na furaha sikuwahi kuifahamu furaha,’’ ’alisema Brouwers aliyetamani kufa kutokana na historia ndefu ya maradhi yake.

“Nilipokuwa na miaka 12 nilipata msongo wa mawazo na nilipofanyiwa uchunguzi niliambiwa kuwa nina maradhi ya akili, nilikuwa sina furaha, mwenye mawazo ya kujikatisha uhai, msongo wa mawazo, mtu nisiye na furaha na mwenye kusikia sauti mithili ya mtu ninayesemeshwa’’.

Madaktari wake hawakuidhinisha maombi yake ya kutaka kukatishwa uhai. Hivyo alipeleka ombi lake kwenye hospitali nyingine mjini The Hague iitwayo Levenseindekliniek yaani ‘Mwisho wa Maisha’. Mahali hapo ni matumaini ya mwisho kwa wale ambao maombi yao yalikataliwa na madaktari wao.

Hospitali hiyo ilikubali kuidhinisha vifo vya watu 65 kati ya 83 wenye matatizo ya akili mwaka jana, ingawa 10% pekee huwa inaidhinishwa na mchakato huu unaweza kuchukua miaka kadhaa.

‘’Wagonjwa wenye matatizo ya akili ni watu wenye umri mdogo, ‘’anasema daktari Kit Vanmechelen, daktari anayewafanyia tathmini waombaji na kukatisha uhai wao, lakini hakuhusika kwenye kifo cha mgonjwa huyo.

‘’Brouwers ni mfano wa mwanamke mwenye umri mdogo. Hivyo inakuwa vigumu kufanya uamuzi wa kukatisha uhai kwa kuwa maisha na ndoto nyingi za mtu zinapotea.

Katika kipindi cha majuma mawili ya mwisho ya uhai wake, Brouwers alikuwa mtu mwenye mawazo sana na alikuwa amejidhuru.

‘’Ninahisi nimefungwa mwilini mwangu, kichwani kwangu, ninataka kuwa huru,’’ alisema.

Brouwers anasema alikuwa anaamini kuwa anaweza kufanya uamuzi lakini je kutamani kwake kufa ilikuwa dalili ya matatizo ya akili?

‘’Nitajuaje-mtu atajuaje kuwa shauku yake ya kufa haikuwa dalili za matatizo ya akili? Daktari anasema kuwa watu hawa wamepoteza matumaini, lakini unaweza kuwasaidia kuwapa matumaini na unaweza kuwaonyesha kuwa huwezi kuwaacha.