Madeni lukuki yakwamisha huduma ya maji

Muktasari:

Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, David Nuntufye alisema licha ya madeni hayo, haijawahi kupata ruzuku kutoka kwa Serikali hivyo kushindwa kutoa huduma kwa ufanisi.

Masasi. Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Masasi-Nachingwea (Manawasa) inazidai taasisi za Serikali wilayani hapa na Nachingwea Sh281 milioni hivyo kushindwa kujiendesha.

Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, David Nuntufye alisema licha ya madeni hayo, haijawahi kupata ruzuku kutoka kwa Serikali hivyo kushindwa kutoa huduma kwa ufanisi.

Alisema wilayani Masasi wanadai zaidi ya Sh134.1 milioni, huku taasisi za Serikali zenye madeni makubwa zikiwa ni Polisi, Hospitali ya Wilaya ya Mkomaindo, Magereza, Jeshi la Wananchi na Ikulu ndogo.

Aliziomba taasisi hizo kulipia maji ili mamlaka iweze kutoa huduma kwa wananchi na hasa wa maeneo ya vijijini.

Mkuu wa Wilaya ya Masasi, Selemani Mzee alisema ameshtushwa na madeni hayo na kuahidi kukutana na wakurugenzi wa halmashauri kuangalia namna ya kuyalipa.

Alisema kuna haja ya kuwa na vikao vya mara kwa mara kati ya ofisi yake na Manawasa ili kupeana taarifa kwa kuwa hilo litasaidia kuweka msukumo wa ulipwaji wa madeni ya huduma ya maji kwa taasisi za Serikali.