Madereva wa Serikali walalamikia posho

Muktasari:

Mwenyekiti wa Chama cha Madereva Mkoa wa Kagera, Steven Bitumbe alisema madereva wa Serikali wanafanya kazi kwa muda na umbali mrefu, lakini hakuna fedha yoyote ya ziada wanayolipwa licha ya kufanya kazi hizo nje ya muda wa kazi.

Karagwe. Madereva wa taasisi za Serikali mkoani Kagera, wamewaomba waajiri kuwalipa stahiki zao na posho za muda wa ziada wa kazi, ili kuondoa changamoto zinazowakabili katika kutekeleza majukumu yao.

Mwenyekiti wa Chama cha Madereva Mkoa wa Kagera, Steven Bitumbe alisema madereva wa Serikali wanafanya kazi kwa muda na umbali mrefu, lakini hakuna fedha yoyote ya ziada wanayolipwa licha ya kufanya kazi hizo nje ya muda wa kazi. Bitumbe alisema kutokana na kazi hiyo, changamoto inayowakabili ni kukosa motisha ya utendaji kutoka kwa waajiri na baadhi yao wanafanya kazi bila kuwa na ajira ya kudumu na kusababisha wakose haki ya kuwkewa mafao ya uzeeni kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii.

“Maofisa wetu wanatutegemea kiusalama tuwapo kwenye uendeshaji magari lakini tunafanya kazi kwa kupewa fedha kidogo katika safari na hata fedha za maegesho tuwapo ugenini tunalazimika kulipa toka mifukoni mwetu,” alisema Bitumbe.

Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe, Ashura Kajuna alisema ukosefu wa posho za madereva na watumishi wengine unatokana na uhaba wa mapato ya ndani ya halmashauri. Aliwaomba madereva hao waendelee kufanya kazi kwa uaminifu, uadilifu na utii wakati tatizo hilo likishughulikiwa.

Wakati huohuo; Ofisa wa Polisi wa Usalama Barabarani wilayani Karagwe, Inspekta Jilala Kisena aliwataka madereva kufanya kazi zao kwa kutii Sheria bila shuruti na kuacha kutoa rushwa kwa askari polisi wanapokuwa na makosa ya kiutendaji ili wawaachie.