Thursday, January 11, 2018

Madereva wa usafiri wa umma hatarini zaidi kuambukizwa TB kuliko abiria wao

 

By Syriacus Buguzi, Mwananchi sbuguzi@mwananchi.co.tz

 Utafiti uliofanywa na wanayasansi wa Taasisi ya Afya ya Ifakara (IHI) umebaini kuwa katika kila mwaka, madereva wa usafiri wa umma jijini Dar es Salaam wako katika hatari kuambukizwa kifua kikuu (TB) mara nane zaidi kuliko abiria wao.

Kwa mujibu wa utafiti huo uliochapishwa katika jarida la afya na maambukizi (Infection Journal), madereva wa usafiri wa umma wako katika hatari kwa asilimia 20.3, wakati abiria wao wako katika hatari kwa asilimia asilimia 2.4.

Hata hivyo, hatari kubwa zaidi imebainishwa miongoni mwa wafungwa, ambao ni asilimia 41.6, ambao ni miongoni mwa makundi yaliyofuatiliwa, ikiwemo majumba ya starehe, makanisa, sehemu za biashara na kumbi za kijamii mfano za harusi.

Majibu ya utafiti huu, hasa kuhusu madereva na abiria wao yanakuja wakati ambapo watu wengi hudhani kwamba kifua kikuu husambaa zaidi miongoni mwa watu walio katika msongamano, hususani magari ya umma. Na wengi, hudhani kwamba abiria wengi ndio wako kwenye hatari zaidi.

Lakini, mtafiti mkuu katika utafafiti huo, Jerry Hella amesema madereva wa umma wanakuwa katika hatari zaidi kwa sababu hutumia muda mwingi ndani ya basi ukilinganisha na abiria wanaoingia na kutoka.

“Kwa siku nzima, uwezekano na muda wa dereva kukaa karibu na abiria mwenye kifua kikuu unaongezeka. Dereva anakuwa na safari nyingi katika basi. Ukilitafiti hili kwa mwaka mzima utagundua kwamba dereva yuko hatarini zaidi kuliko abiria wanaoingia tu na kutoka,’’ amesema.

Wafungwa je?

“Miongoni mwa wafungwa ambao huongoza kwa kuwa katika hatari, tumebaini kuwa wengi wanakuwa ni watu kutoka kipato cha chini. Wanakuwa ni watu wenye lishe duni, wamedhoofu. Ukizingatia kwamba mazingira ya jela yanakuwa si masafi na pia ni duni, hii huongeza uwezekano wa kupata kifua kikuu mara dufu ukilinganisha na watu wengine katika jamii,’’ alibainisha.

“Tulifanya utafiti huu kwa hapa Dar es Salaam kwa sababu ni jiji linaloongoza kwa visa vya kifua kikuu vinavyoripotiwa katika programu za kupambana na kifua kikuu. Pia ni jiji linalokua kwa kasi zaidi barani Afrika. Lakini pia, kazi zetu nyingi za utafiti tunafanyia maeneo ya miji,” aliongeza.

Hatari maeneo mengine

Maeneo mengine yaliyobainika kuwa na hatari ya mtu kuambukizwa vimelea vya TB na asilimia katika mabano ni masoko makubwa (4.8), miongoni mwa wafanyabiashara na wateja wao (0.5) na abiria katika usafiri wa umma (2.4). Pia, watafiti wamebainisha kuwa hatari ya maambukizo katika shule za umma ni asilimia 4.0, klabu za burudani (1.7), majengo ya ibada (0.13), kumbi za kijamii (0.12).

Utafiti utatatua changamoto?

“Majibu haya yatasaidia wadau na Serikali katika kujua maeneo ambayo wanapaswa kuwekeza zaidi ili kutokomeza kifua kikuu kulingana na mpango wa Shirika la Afya Duniani (WHO),’’ alisema Hella. Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, ugonjwa wa kifua kikuu maarufu kama TB huambukizwa kwa njia ya hewa.

Watafiti walikusanya takwimu kwa kutumia teknolojia mpya. Walikusanya hewa ya carbondioxide ambayo watu hutoa nje wakati wa kupumua. Walikusanya hewa hiyo katika magari, majumbani, sehemu za starehe, makanisani na kwenye nyumba za mahabusu.

Na baada ya hapo wakaifanyia uchanganuzi wa kitaalamu (analysis) na kubaini chembe za TB.

“Unajua, vimelea vya TB huambukizwa pale mgonjwa anapokohoa hewa yenye hivyo vimelea vikiwa katika mfumo wa chembechembe (particles),’’ anaeleza.

“Hizi chembechembe zikiingia katika hewa wanayovuta watu zinaweza kupotea endapo hewa safi itakuwa katika kiwango kikubwa kwenye mzunguko. Lakini kama hewa safi hakuna, hasa katika maeneo yenye msongamano mkubwa au nyumba zisizo na uingizaji hewa mzuri, watu waliopo katika hayo maeneo wanakuwa katika hatari kubwa ya kuambukizwa,’’ aliongeza.     

-->