Madiwani, Naibu Meya Chadema wakamatwa na polisi Arusha

Muktasari:

Meya wa Jiji la Arusha, Kalist Lazaro amesema Viola na madiwani hao wawili walikamatwa wakiwa katika mkutano wa ndani uliokuwa ukisikiliza kero za wananchi.

Arusha. Naibu Meya wa Jiji la Arusha, Viola Likindikoki na madiwani wengine wawili wa Chadema wamekamatwa na jeshi la polisi mjini hapa kwa sababu ambazo mpaka sasa hazijafahamika.

Meya wa Jiji la Arusha, Kalist Lazaro amesema Viola na madiwani hao wawili walikamatwa wakiwa katika mkutano wa ndani uliokuwa ukisikiliza kero za wananchi.

“Nipo Tanga kikazi na nilimkaimisha nafasi yangu Viola, kwa kawaida Alhamisi tunasikiliza kero za wananchi, wakati wakiendelea kusikiliza kero ndipo walipokamatwa,” alisema Lazaro.

Wengine waliokamatwa katika tukio hilo ni diwani wa viti maalumu (Chadema)Kata ya Ngarenaro, Happiness Charles na diwani wa Viti Maalumu Kata ya Olorieni Sabrina Francis.

Kamanda wa Polisi mkoani Arusha, Charles Mkumbo amethibitisha kushikiliwa viongozi hao na kusema kwa kifupi kwamba jeshi lake linawashikilia kwa uchunguzi.

Akizungumza na gazeti hili jana, diwani wa Viti Maalumu (Chadema), Jenipher Lomayan alisema madiwani hao walikamatwa jana saa 9 alasiri wakiwa ndani ya ofisi ya Meya wa Jiji la Arusha wakisikiliza kero za wananchi.

Lomayan alisema wakiwa ndani ya ofisi hizo polisi waliovalia nguo za kiraia waliingia na kuwaeleza kwamba wako chini ya ulinzi na wanatakiwa kufika mbele ya makao maku ya jeshi hilo kwa uchunguzi zaidi.

“Wale polisi walitaka kuichukua simu ya Naibu Meya na ndipo madiwani wawili(Sabrina na Happiness) waliingilia kati na kuwazuia polisi wasimnyang’anye simu hiyo na ndipo na wao wakaunganishwa katika tukio hilo,” alisema.