Madiwani CUF wageuka mabondia

Askari waliovalia nguo za kiraia wakimtuliza mfuasi wa chama cha CUF baada ya kutokea vurugu katika ofisi ya chama hicho ya wilaya ya Tanga jana. Picha na Raisa Said

Muktasari:

  • Makundi hayo ya madiwani yaligawanyika  kuhusu uamuzi wa wenzao waliohudhuria kikao cha baraza la madiwani wa jiji hilo Oktoba 12.

Tanga. Polisi mjini hapa jana walilazimika kuingilia na kuzima vurugu zilizotokea katika ofisi za Chama cha Wananchi (CUF), Wilaya ya Tanga zilizotokana na madiwani kugawanyika katika makundi mawili.

Makundi hayo ya madiwani yaligawanyika  kuhusu uamuzi wa wenzao waliohudhuria kikao cha baraza la madiwani wa jiji hilo Oktoba 12.

Vurugu zilianza baada ya Mwenyekiti wa CUF wilayani humo, Rashid Jumbe ambaye pia ni diwani wa Mwanzage aliyegombea nafasi ya umeya kuamuru madiwani waliohudhuria baraza hilo watoke nje ili wajumbe waanze kumjadili mmoja mmoja.

Baada ya amri hiyo kundi la madiwani 12 waliotolewa nje kusubiri kuhojiwa waliamua kuingia kwa nguvu kutaka kumtoa Jumbe wakidai anasababisha makundi ndani ya chama hicho.

Vurugu ziliendelea kwenye mlango wa kuingilia, jambo lililosababisha wanachama waliokuwa nje kuingilia kati, huku wakirushiana ngumi.

Baadaye magari matatu ya polisi yaliwasili katika ofisi hizo na kuwatawanya wanachama waliokuwa wamejaa, jambo lililomsaidia Jumbe kufanikiwa kutoka.