Madiwani watumia mkutano kupigana vijembe

Muktasari:

  • Meya Mwita asema maendeleo hayana vyama.

 Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita amelazimika kuingilia kati kuwatuliza wajumbe wa baraza la madiwani la jiji hilo waliokuwa wakipigana vijembe kwa misingi ya vyama.

Wajumbe waliokuwa kwenye kikao cha kupitia utelezaji wa bajeti ya mwaka 2016/17 walitumia muda mwingi kusifia vyama vyao badala ya kujikita kwenye hoja iliyo mbele yao.

Mbunge wa Temeke, Abdallah Mtolea aliposimama alihoji ni kwa nini chumba chao cha mikutano hakina vipaza sauti wakati bajeti iliyopita ilihusisha ukarabati.

Mkurugenzi wa Jiji, Sipora Liana alimjibu kuwa fedha zilikwisha lakini jitihada zinaendelea ili vipaza sauti vipatikane.

Aliposimama diwani wa Kibondemaji, Abdallah Mtinika alimpongeza meya Mwita ambaye ni diwani wa Chadema kwa kutekeleza ilani ya CCM.

"Nikupongeze meya, tunaona ilani ya CCM inatekelezwa kwa vitendo mambo yanakwenda sawa na ndiyo sababu leo mtu anasimama anakosa la kusema matokeo yake anaulizia vipaza sauti," alisema.

Kauli hiyo ilimuinua diwani wa Tabata, Patrick Asenga aliyekanusha kutekelezwa ilani ya CCM katika Jiji la Dar es Salaam.

"Nikupongeze meya kwa kuwa kwa mara ya kwanza Jiji la Dar es Salaam mambo yanakwenda sasa hiyo ni kutokana na uongozi imara wa Ukawa, hakuna mambo ya CCM hapa," alisema Asenga.

Meya Mwita aliingilia kati na kuwataka madiwani kujikita kwenye hoja zilizomo kwenye makabrasha.

Akizungumza na MCL Digital baada ya kikao hicho leo Februari 23,2018 Meya Mwita amesema anatambua maendeleo hayana vyama na lengo lake ni kuifanya Dar es Salaam iwe jiji lenye maendeleo zaidi.

"Ukitaka mambo yaende vizuri, wakati mwingine hutakiwi kuipa nafasi sana siasa ndiyo sababu sina ubaguzi, nataka madiwani wote wawe kitu kimoja kwa ajili ya maendeleo," amesema Mwita.