Madiwani Kino wawapoka vyeo wahandisi watatu

Meya wa Kinondoni, Boniface Jacob

Muktasari:

Watumishi hao walisimamishwa kazi mwaka jana baada ya manispaa hiyo kubaini walikiuka wajibu wao na kuamuru iundwe timu ya kuchunguza madai hayo dhidi yao.

Dar es Salaam. Baraza la Madiwani wa Manispaa ya Kinondoni limeamuru kushushwa vyeo na kuwakata mishahara wafanyakazi tisa wakiwamo wahandisi watatu kwa kushindwa kutumia taaluma yao kutoa ushauri kwenye ujenzi wa barabara.

Watumishi hao walisimamishwa kazi mwaka jana baada ya manispaa hiyo kubaini walikiuka wajibu wao na kuamuru iundwe timu ya kuchunguza madai hayo dhidi yao.

Uamuzi huo wa kuwashusha madaraja na kuwakata mishahara umechukuliwa baada ya baraza hilo kupokea ripoti ya uchunguzi ya timu zilizoundwa na manispaa hiyo,  ikiwamo ya kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya.

Akitangaza uamuzi wa Baraza la Madiwani lililokutana juzi, Meya wa Kinondoni, Boniface Jacob alisema limejiridhisha kuwa watumishi hao wametenda makosa hayo na kuisababishia manispaa hiyo hasara katika ujenzi wa barabara.