Madiwani Simanjiro wapitisha rasimu ya mpango wa bajeti ya Sh25.3bilioni

Muktasari:

Akizungumza jana Januari 20,2018 mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Jackson Sipitieck amesema vipaumbele vya bajeti hiyo ni elimu, afya, maji na viwanda. 

Simanjiro. Baraza la madiwani halmashauri ya wilaya ya Simanjiro mkoa wa Manyara  limepitisha rasimu ya mpango wa bajeti ya Sh25.3 bilioni kwa mwaka wa fedha 2018/19. 

Akizungumza jana Januari 20,2018 mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Jackson Sipitieck amesema vipaumbele vya bajeti hiyo ni elimu, afya, maji na viwanda. 

Amesema  kupitishwa kwa bajeti ni jambo moja na utekelezaji ni jambo lingine, kutaka kila diwani kuhakikisha wanatimiza wajibu wao ili kufanikisha suala hilo.

“Kila mmoja akisimama kwa nafasi yake wilaya ya Simanjiro itapiga hatua kubwa kimaendeleo na wananchi  watapata huduma  za kijamii kwa ufanisi mkubwa zaidi,” amesema. 

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo, Yefred Myenzi amesema bajeti hiyo ni kwa ajili ya matumizi mbalimbali, ikiwemo miradi ya maendeleo, ruzuku ya uendeshaji ofisi na mishahara. 

Myenzi amesema wilaya hiyo imeweka mikakati ya kuhakikisha wanaboresha vipaumbele vyao vya elimu, afya, maji na viwanda. 

“Mazao ya mifugo ikiwemo maziwa, ngozi na nyama inapaswa kuboreshwa ili iwe chachu ya vichocheo vya uchumi kwa jamii,” amesema.

Katibu Tawala wa wilaya ya Simanjiro, Zuwena Omary amewapongeza madiwani wa halmashauri hiyo kwa kupitisha mpango huo, “Pamoja na hayo tunapaswa kuhakikisha tunatekeleza agizo la kila mkoa kuwa na viwanda 100 kwa sisi Simanjiro kuanzisha viwanda 15 ambayo vitasambazwa kwenye kata zetu na vijiji."