Madiwani Tarime wawaadhibu viongozi waliosababisha hasara ya mamilioni

Muktasari:

Akitoa taarifa ya hatua iliyochukuliwa na kamati ya maadili ya utumishi, mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Hamis Nyanswi amewataja waliochukuliwa hatua hizo kuwa ni Simion Nyadwera aliyekuwa katibu wa idara ya afya ambaye alihamishiwa katika Halmashauri ya Maswa anadaiwa kuchota Sh24 milioni na ametakiwa kurejesha kiasi hicho cha fedha huku Taasisi ya Kuzuia  na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ikitakiwa kumchunguza utumishi wake.

Tarime. Baraza la Madiwani la Halmashauri ya mji wa Tarime mkoani Mara leo Alhamisi, Agosti 17 limewakuta na hatia na kuwachukulia hatua za kisheria watumishi wanne kwa kutumia vibaya madaraka yao na kuisababishia halmashauri hiyo hasara ya mamilioni ya fedha.

Akitoa taarifa ya hatua iliyochukuliwa na kamati ya maadili ya utumishi, mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Hamis Nyanswi amewataja waliochukuliwa hatua hizo kuwa ni Simion Nyadwera aliyekuwa katibu wa idara ya afya ambaye alihamishiwa katika Halmashauri ya Maswa anadaiwa kuchota Sh24 milioni na ametakiwa kurejesha kiasi hicho cha fedha huku Taasisi ya Kuzuia  na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ikitakiwa kumchunguza utumishi wake.

Nyanswi amemtaja mtuhumiwa mwingine kuwa ni Laurenti Marwa aliyekuwa afisa utumishi Mwandamizi wa Halmashauri ya Mji wa Tarime aliyedaiwa kushirikiana na watumishi 60 kuzisababishia hasara taasisi za fedha na kuiingiza halmashauri hiyo kwenye mgogoro mkubwa.

Amesema kuwa Marwa atapunguziwa mshahara wake kutoka ngazi ya mshahara ya TGTS F yenye kiwango cha mshahara wa Sh1.3 milioni kwenda TGTS E, yenye kiwango cha mshahara wa Sh950,000.

"Pamoja na adhabu hiyo Marwa atatakiwa kuzilipa cha Sh26 milioni alizosababishia hasara taasisi hizo," amesema Nyanswi.

Watumishi wengine ni Sabure Masanja na Quinter Wayoga waliopewa onyo kutokana na makosa yao.

"Walikuwa akichelewa na pia kuwahi kuondoka kazini na kusababisha usumbufu mkubwa kwa wananchi kukosa huduma yake," amesema mwenyekiti huyo.

Watumishi hawa hawakuwa tayari kuzungumzia uamuzi uliochukuliwa na baraza la madiwani licha ya kupigiwa simu na kuita bila kupokelewa.

Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko amewataka watumishi wa umma kuzingatia maadili ya kazi zao ili kuwafanya wananchi kupata huduma wanayostahiki badala ya kukutwa na usumbufu usio kuwa wa lazima.

"Watumishi wa umma wasimamie vizuri nafasi zao ili kuepukana na matatizo yanayowafanya kuanza kufuatiliwa na waajiri wao, nasi kama baraza la madiwani hatutasita kuwachukulia hatua za kinidhamu pale majina yao yanapofikishwa kwetu," amesema Matiko.