Madiwani waikalia kooni GGM

Geita/Bukombe. Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita limetishia kukata mabomba yanayopeleka maji katika mgodi wa Kampuni ya Geita Gold Mine (GGM) endapo haitaridhia kulipa deni la Dola 11 milioni za Marekani.

Pia, limesema litazuia magari kupita barabarani kama haitalipa malimbikizo ya kodi hayo ya deni tangu mwaka 2004 hadi 2013.

Hata hivyo, Meneja wa Kitengo cha Uhusiano GGM, Joseph Mangilima aliwataka madiwani hao kutambua kuwa maji wanayotishia kukata wamepewa na bonde la ziwa victoria na si halmashauri.

Pia, alisema wamekuwa wakilipa Sh60 milioni kila mwaka kama ada ya kutumia maji katika ziwa hilo.

Akizungumza katika baraza hilo, mbunge wa Busanda, Lolensia Bukwimba alisema ni vyema wakatangaza mgogoro na kukata mawasiliano baina ya Serikali na mgodi huo.

Bukwimba alisema hayo baada ya mwenyekiti wa baraza hilo, Elisha Lupuga kutoa taarifa ya majibu ya barua waliyotumiwa wawekezaji hao waliotakiwa kulipa deni hilo ndani ya siku 30 na kujibu hawatalipa na wapo tayari kukutana mahakamani.

Lupuga alisema katika barua iliyopelekwa GGM Julai 27 ya kuitaka ilipe deni hilo uongozi wa mgodi ulipinga kulipa.

“Suala la kwenda mahakamani ni baadaye sisi tutakata mabomba yao maana maji wanachukua kwetu, hawawezi kutuonyesha jeuri juu ya sheria zetu,” alisema Bukwimba.

Wakizungumza katika kikao hicho diwani wa Busanda, Elias Kasome na Roza Musa wa viti maalumu kutoka Butundwe, walisema wataungana na wananchi kuzuia magari ya GGM yasipite.

Mwanasheria wa halmashauri hiyo, Allan Shija alisema fedha hizo zinatokana na kodi ya huduma.

Alisema mgodi wa GGM ulianza uzalishaji mwaka 2000 na kuingia makubaliano na Wizara ya Nishati na Madini ya kulipa Dola 200,000 za Marekani kwa halmashauri kila mwaka.

Mkuu wa Wilaya ya Geita Herman Kapufi aliwataka madiwani hao kuwa watulivu na kuahidi kukaa kikao na uongozi wa GGM ili kuona namna ya kuafikiana.