Madiwani waliojiuzulu Chadema waanguka kura ya maoni CCM

Muktasari:

Viongozi wa CCM wamesema mchakato bado unaendelea.

Arusha. Madiwani watatu wa Chadema waliojiuzulu katika Halmashauri ya Meru mkoani Arusha na kujiunga na CCM, wameangushwa katika kura ya maoni ndani ya chama hicho.

Madiwani hao waliojiuzulu hivi karibuni kwa kile walichoeleza ni kutokana na kuunga mkono jitihada za Rais John Magufuli waliomba kutetea nafasi zao.

Waliogombea na kuangushwa ni Solomon Laizer, aliyekuwa diwani wa Ngabobo, Japhet Jackson (Embuleni) na Anderson Sikawa (Leguruki).

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Meru, Andrew Mungure amesema leo Jumatano Oktoba 18 kuwa, matokeo ya kura ya maoni si mwisho wa uteuzi. Uchaguzi huo ulifanyika jana Jumanne.

Mungure amesema wagombea katika kata hizo watajulikana baada ya vikao ambavyo vimeanza leo.

"Leo wanajadiliwa wagombea wote ngazi ya kata, baadaye tutajadili kamati ya siasa na halmashauri kuu ya mkoa ndipo watapitishwa wagombea," amesema.

Amesema kutokana na mchakato huo, matokeo ya kura ya maoni si mwisho.

Katibu wa CCM Wilaya ya Meru, Aloyce Hayuma amekiri madiwani hao kugombea na kushindwa. Hata hivyo, amesema mchakato unaendelea.