Mbarawa amjia juu Saada Mkuya

Muktasari:

  • Waziri Mbarawa amesema hakutegemea Mkuya aseme maneno aliyoyatoa bungeni

Serikali imemjia juu waziri wa zamani wa Fedha, Saada Mkuya kwa kutoa mapendekezo ya kutaka ajira kwa shirika la mawasiliano la simu kwa upande wa Zanzibar ziwe kwa Wazanzibar.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amesema alitegemea hoja ya aina hiyo ingezungumza na watu vijijini huko Pemba au vijiweni huko darajani Zanzibar na siyo Mkuya.

Profesa Mbarawa aligeuka mbogo leo Jumatatu jioni wakati akijibu hoja mbalimbali za wabunge waliochangia Muswada wa Shirika la Mawasiliano wa 2017, uliowasilishwa na Profesa Mbarawa.

“Utaratibu wa ajira TTCL ni Mtanzania yeyote anafanya kazi TTCL. Tunachoangalia sisi muhimu ni uwezo wa mtu na sifa za mtu. Jambo alilolisema Saada Mkuya limenisikitisha sana,” amesema.

“Sikutegemea maneno hayo yangetoka kwa kiongozi kama Saada ambaye alikuwepo serikalini. Hasa kwa kiongozi ambaye ana uzoefu mkubwa,” amesema Profesa Mbarawa na kuongeza kuwa;

“Nilitegemea mawazo au maoni kama yale yazungumzwe na watu wa kijijini kule Pemba. Nilitegemea mawazo kama yale yazungumzwe na watu wa kijiweni pale Darajani,”

“Nilitegemea yeye kama kiongozi na sisi kama Tanzania katika kujenga umoja wetu tuseme kila Mtanzania afanye kazi mahali popote Tanzania,”

“Mheshimiwa Naibu Spika hivi tunavyoongea leo, Meneja wa TTCL Zanzibar ni Mzanzibar anaitwa Mohamed Mohamed. Meneja wa TTCL Pemba ni Mnzanzibar anaitwa Ngwali Hamis,”

“Naomba nimpe taarifa mheshimiwa Saada ambaye hazijui kiutendaji.  Mtendaji Mkuu wa TTCL mwaka 2010 hadi 2012 alikuwa Injinia Said Ameir ni Mzanzibar,”

“Sasa sikutegemea nasema ni kitu kimeniuma sana. Nilitegemea kama Mtanzania unatoka Lindi kama kuna fursa TTCL Zanzibar unaenda. Kama Mzanzibar ameona fursa Kibondo aende.”

“Hii ndio Tanzania tunayoitaka. Hii ndio Tanzania ambayo Watanzania kule nje wanaitaka. Nikienda zaidi TTCL tuna TTCL Pesa ina watendaji watano waandamizi. Watatu ni wanzanzibar”

Jitihada za Saada kutaka kumpa Profesa Mbarawa taarifa ziligonga mwamba baada ya Naibu Spika kumweleza kuwa kikanuni waziri akiwa amesimama kwa hatua ya jana, hakuna taarifa.