Mafataki yakatisha ndoto za wanafunzi 42

Muktasari:

Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Nurdin Babu katika mkutano wake na wakazi wa mji wa Mugumu alimwagiza kamanda wa polisi wilayani humo kuwakamata wanaume wanaodaiwa kuwapa ujauzito wanafunzi hao na kuwafikisha mahakamani.

Serengeti. Serikali wilayani Serengeti, Mkoa wa Mara imeapa kupambana na wanaume waliowakatishia masomo wanafunzi wa kike zaidi ya 42 wa shule za msingi na sekondari kwa kuwapa ujauzito.

Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Nurdin Babu katika mkutano wake na wakazi wa mji wa Mugumu alimwagiza kamanda wa polisi wilayani humo kuwakamata wanaume wanaodaiwa kuwapa ujauzito wanafunzi hao na kuwafikisha mahakamani.

Pia, aliagiza wazazi wa wanafunzi hao ambao wanawalinda waliowapa ujauzito wakamatwe na kufikishwa mahakamani.

“OCD kamata wazazi na watoto ambao watajaribu kuficha ukweli na wafikishwe mahakamani kwa kuwa kumeibuka mtindo wa wazazi kushirikiana na watoto na anapoulizwa aliyempa mimba hamjui, wenye majibu kama hayo kamata wote,” alisema Babu.