Mafuriko yasomba nyumba 36

Muktasari:

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutembelea eneo la tukio juzi, Mkuu wa Wilaya ya Busega, Tano Mwera alisema pamoja na kubomoa nyumba za wananchi, mafuriko hayo pia yameharibu miundombinu ya barabara, madaraja na viwanja vya michezo.

Watu zaidi ya 100 kutoka kaya 36 za Kata ya Lamadi wilayani hapa mkoani Simiyu hawana makazi baada ya nyumba zao kubomolewa na mafuriko yaliyotokana na mvua za masika zinazoendelea kunyesha mkoani hapa.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutembelea eneo la tukio juzi, Mkuu wa Wilaya ya Busega, Tano Mwera alisema pamoja na kubomoa nyumba za wananchi, mafuriko hayo pia yameharibu miundombinu ya barabara, madaraja na viwanja vya michezo.

“Waathirika wa tukio hili wamehifadhiwa katika makazi ya ndugu, jamaa na marafiki huku Serikali ikiendelea kufanya tathmini kujua madhara na misaada ya haraka inayohitajika,” alisema Mwera.

Aliwataka wananchi wanaoishi maeneo ya mabondeni kuchukua tahadhari kutokana na utabiri wa hali ya hewa kuonyesha uwapo wa mvua kubwa katika msimu huu.

Mkazi wa kitongoji cha Kisesa Mariamu Juma ambaye ni miongoni mwa waathirika, alisema nyumba yake ilianguka baada ya kuzingirwa na maji ya mafuriko.

Hata hivyo, aliishukuru Serikali kwa juhudi za haraka za kuokoa maisha yao.

Mwathirika mwingine, Samuel Mathayo aliwasihi wanaoishi mabondeni kuhama hadi hapo mvua zitakapopungua ili kunusuru maisha na mali zao.