Mafuta ya magendo yakamatwa

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Benedict Wakulyamba

Muktasari:

  • Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Benedict Wakulyamba alisema wameamua kuchukua hatua zaidi baada ya kutaifisha mali zinazokamatwa kwa kuingizwa kwa magendo, hivyo wanaanza kuwafungulia kesi za uhujumu uchumi.

Tanga. Polisi imekamata madumu 1,606 ya kupikia yenye ujazo wa lita 20 kila moja yaliyoingizwa nchini kwa magendo kupitia Bandari Bubu ya Kwale wilayani Mkinga.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Benedict Wakulyamba alisema wameamua kuchukua hatua zaidi baada ya kutaifisha mali zinazokamatwa kwa kuingizwa kwa magendo, hivyo wanaanza kuwafungulia kesi za uhujumu uchumi.

Wakulyamba alisema kuwa mafuta hayo aina ya Shakila yanayosadikiwa kutoka nchini Malaysia, yalikamatwa juzi saa tano usiku katika Bandari Bubu ya Kwale.

Inaelezwa kuwa mafuta hayo yalikuwa yamepakiwa kwenye magari mawili aina ya Fuso. Alisema magari hayo yalikuwa yamebeba madumu 1,606 na kwamba, magari na mizigo hiyo vimekabidhiwa kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa hatua zaidi. Alisema watu watano waliokuwamo kwenye magari hayo ambao ni wakazi wa Muheza, Kisiwani Pemba na Tanga Mjini wanashikiliwa na polisi.

“Tunawakamata madereva wa magari yanayokutwa na bidhaa za magendo au manahodha wa vyombo vya baharini, ambao na wakati mwingine hukimbia kwa kuzamia majini lakini wamiliki wa bidhaa wanaendelea na shughuli zao, sasa tutawakamata na kuwafungulia kesi za uhujumu uchumi,” alisema Wakulyamba.

Wakati huohuo, watu wawili wamekutwa wamekufa wakiwa kwenye nyumba ya kulala wageni huku miili yao ikiwa chumba kimoja imefungwa kamba mikononi, tumboni na miguuni. Wakulyamba alisema tukio hilo linatatanisha kwa sababu miili ya watu hao haikuwa na majeraha, bali michubuko midogo ya kufungwa kamba.