Magereza kufufua kiwanda cha sukari Mbigiri

Kaimu Kamishna wa Magereza nchini,Dk Juma Malewa kulia akiwaonyesha wanahabari mkataba wa makubaliano kwa ajili ya kufufua kilimo cha  miwa na kiwanda cha  sukari cha Gereza la Mbigiri lililopo Morogoro.Kushoto ni Kaimu mkurugenzi mkuu wa kampuni tanzu ya Mkulazi , Nicander Kileo watakaoshirikiana katika mchakato huo. Picha na Bakari Kiango

Muktasari:

Makubaliano yalisainiwa leo (Ijumaa)  kati ya Kaimu Kamishna wa Magereza nchini, Dk Juma Malewa na wakurugenzi watendaji wa mifuko hiyo kwenye ofisi ya makao makuu ya jeshi jijini hapa.

Dar es Salaam. Jeshi la Magereza nchini, limeingia mkataba wa makubaliano na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya PPF na NSSF, kwa ajili ya kufufua kilimo cha miwa na kiwanda cha sukari cha Gereza la Mbigiri lililopo Morogoro.

Makubaliano yalisainiwa leo (Ijumaa)  kati ya Kaimu Kamishna wa Magereza nchini, Dk Juma Malewa na wakurugenzi watendaji wa mifuko hiyo kwenye ofisi ya makao makuu ya jeshi jijini hapa.

Kabla ya kusaini makubaliano hayo, Dk Malewa amewaeleza wanahabari kuwa huo ni mkakati mmoja wapo wa kuhakikisha magereza linajitegemea sanjari na kuunga mkono juhudi za Serikali za kuwa  nchi ya viwanda

"Tumedhamiria kuanzisha kilimo cha miwa katika shamba letu la Mbigiri, hatua hii itatuwezesha kuwa na sukari ya kutosha kwa ajili ya magereza na itakayobaki tutaiuza," amesema Dk Malewa.