Megereza waanza kujipanga kwa viwanda, kilimo

Muktasari:

Amesema uzalishaji katika viwanda hivyo utakuwa maradufu na wameshajihakikishia uhakika wa masoko ndani na nje ya Tanzania hususan kwa upande wa viatu.


Morogoro. Kamishna Jenerali wa Magereza, Dk Juma Malewa amesema jeshi hilo limeanza kutekeleza maelekezo ya Rais John Magufuli ya Tanzania ya viwanda, kwa kuanzisha na kupanua viwanda vipya kikiwamo cha kutengeneza viatu kilichopo gereza la Karanga mkoani Kilimanjaro na cha sukari katika gereza la Mbigiri Morogoro.

Amesema uzalishaji katika viwanda hivyo utakuwa maradufu na wameshajihakikishia uhakika wa masoko ndani na nje ya Tanzania hususan kwa upande wa viatu.

Dk Malewa ametoa kauli hiyo jana Jumapili Machi 18, 2018 baada ya kumaliza kikao kazi cha dharura kilichofanyika mjini Morogoro kikiwahusisha maofisa waandamizi wa Magereza.

“Nimelazimika kuitisha kikao kazi hiki cha dharura kwa maofisa ili tuweze kubainisha mahitaji makubwa yaliyo mbele yetu ikiwamo nguvu kazi na vitendea kazi hasa matrekta ili kuongeza nguvu ya kilimo, kwa sasa tunamudu kulisha wafungwa kwa asilimia 30 tu,”amesema.