Magufuli: Wasaidizi wangu wameanza kunielewa

Mfanyabiashara mdogo mjini Morogoro, Mama Havintoshi akichangiwa fedha na viongozi na wageni mbalimbali baada ya kuwasilisha kero yake kwa Rais John Magufuli, kuhusu kunyanyaswa wakati akifanya biashara zake katika kituo cha daladala mjini mjini. Dk Magufuli pia alimchangia mama huyo sh100,000 katika hafla ya ufunguzi wa kiwanda cha Sigara cha Mansoor Industries ltd kilichopo chini ya leseni ya Phillip Morris Tanzania katika eneo la Kingolwira mkoani humo jana. Picha na Ikulu

Muktasari:

Kauli hiyo ya Magufuli imekuja miezi kadhaa tangu aseme wasaidizi wake hawamuelewi, hawaelewi Bunge linataka nini na mahitaji ya Watanzania.

Rais John Magufuli amesema sasa wasaidizi wake wameanza kumuelewa.

Kauli hiyo ya Magufuli imekuja miezi kadhaa tangu aseme wasaidizi wake hawamuelewi, hawaelewi Bunge linataka nini na mahitaji ya Watanzania.

Januari mwaka huu, wakati akimuapisha Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko, Rais Magufuli alisema; “...Baadhi ya ninaowateua bado hawajanielewa na hawajaelewa Bunge linataka nini, Watanzania wanataka nini.”

Miongoni mwa viongozi walionyooshewa vidole hadharani kwa utendaji wao siku hiyo ni Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage kwa kushindwa kurejesha serikalini viwanda vilivyobinafsishwa lakini havifanyi kazi,

Lakini, jana kwa kumtumia waziri huyohuyo, alisema sasa anashukuru kwamba watendaji hao wameanza kumuelewa.

Akizindua Kiwanda cha Sigara cha Phillip Moris kilichopo, Kingolwira, Morogoro jana, Rais Magufuli alimwambia Mwijage, “Kuna wakati ulikuwa kidogokidogo na kweli nilikasirika tatizo nililonalo mimi ni kusema ukweli, lakini viongozi sasa wananielewa ukiwemo mheshimiwa Mwijage.”

Aliwataka watendaji hasa viongozi kutokuwa watengeneza kero, badala yake wawe watatuzi wa kero akibainisha kuwa kuna mambo ambayo hayahitaji kumfikia akitolea mfano malalamiko ya watu kuhusu kodi, kudhulumiwa ardhi akisema yatakwisha iwapo kila mtendaji atasimamia haki na kujua nafasi yake ya kazi anayoifanya kwa niaba ya Watanzania wote.

“Nawaombeni wakuu wa wilaya, wakurugenzi, maofisa tarafa na watendaji wa kata... kila mmoja katika kazi zao wajitahidi kuwa watatuzi wa kero na wasiwe watengeneza kero,” alisema Magufuli.

Mbali na kuzungumzia ufanisi wa utendaji wa Serikali katika kufufua na kuanzisha viwanda, Rais Magufuli pia alizungumzia umuhimu wa kutunza amani huku akivipongeza vyombo vya ulinzi na usalama na kuviambia, “Wakati mwingine mnatukanwa na watu wasiowajua kwamba kula kwao na kushiba kwao kunawategemea ninyi.

“Unajua na amani huwa inalevya kila kitu huwa kinalevya ukila ugali sana utalewa, ukila wali sana utalewa, chochote ukila sana utalewa... wanashindwa kuelewa kwenye nchi kama Iraq ambapo unamuona mtoto amepigwa risasi amekufa, mtu alikuwa na nyumba yake amewekeza kwa mabilioni limebomolewa ...walitaka iwe hivyo, wanashindwa kuelewa wale walichezea amani.”

Alisema mfano ni katika nchi jirani wanawaona watu wanakimbia wapo tayari wazame kwenye maji hata Libya iliyokuwa nchi nzuri wapo radhi wakafe kwenye Bahari ya Mediterranean wanakimbilia Ulaya... “Unafikiri walihitaji hicho? Kimewapata kwa sababu ya kuchezea amani.

“Ukichezea amani umechezea maisha yako, unaweza ukafikiri wewe upo mbali lakini litakupata tu, lisipokupata wewe, litampata hata ndugu yako, litampata hata shangazi yako, hata mjukuu wako.

“Angalieni majirani zetu yanayowapata liwe funzo tusi-test chakula ambacho hakiliki.”

Alisema amani iliyopo ndiyo itakayoleta wawekezaji kwani hawawezi kwenda katika nchi ambayo watu wanapigana kila siku.

Akizungumzia kiwanda hicho, alisema uwepo wake utawahakikishia wakulima wa Morogoro na maeneo mengine yanayolima tumbaku soko zuri na la uhakika.

Alisema siku za nyuma mkoa huo ulikuwa na viwanda vingi na kuwavutia watu wengi waliokuwa wanataka ajira, lakini ilifika mahali Watanzania wakaingiliwa ugonjwa mbaya wa kusahau viwanda vyao na kuviua kwa kuweka bodi ambazo zilisababisha vife... “Tumejifunza, mara nyingi kujifunza unajifunza kwa makosa, yasirudiwe tena.”

Alisema kuua kiwanda kama hicho maana yake ni kuua zao la tumbaku kama ilivyo kwa kuua kiwanda cha pamba.

Alisema viwanda ni kichocheo cha ajira akitolea mfano wa wafanyakazi 224 na kuhoji, “Wasingekuwa na kazi wangekuwa wanafanya nini? Kwa sababu wana familia - hivyo faida ya kuwa na kiwanda ni pamoja na kupanua kipato chao.”

Aliwataka Watanzania wabadilike na kuwa na mtazamo wa kuwa na viwanda vya kutosha kwa sababu ndiyo njia pekee ya kupunguza tatizo la ajira akisema viwanda vilivyoachwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere vingekuwapo kusingekuwa na tatizo la ajira.

Ampa wakati mgumu RC

Akijibu ombi la Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Kebwe Stephen Kebwe aliyeomba wananchi wapewe eneo la msitu wa hifadhi, Magufuli alisema anapata kigugumizi kuvunja Katiba aliyoapa kuilinda.

“Ninafahamu mkuu wa mkoa anaomba eneo la misitu lililohifadhiwa na tayari eneo hilo limeshajengwa nyumba zaidi ya 1,000. Wakati hayo yanafanyika mkuu wa mkoa alikuwepo, mkuu wa wilaya alikuwepo... zinajengwa wanatazama tu hata kuwaeleza hili ni hifadhi la pori la mkoa huu wanatazama tu, ofisa ardhi anatazama tu, zimejengwa nyumba zaidi ya 1,000 leo anakuja kuniomba...

“Ungekuwa wewe ni Rais ungesemaje? Kuna nyumba hata ya mkuu wa mkoa au wa wilaya amejenga kule, ndiyo maana nawauliza, nimepongeza hatua za kufuta yale mashamba pori, nilisema wapewe wananchi bure, wagawiwe yale ni mashamba yao walidhulumiwa miaka ya nyuma.

Alisema anafahamu kwamba ameletewa ombi hilo kwa sababu aliruhusu watu wa Kahama wakae katika maeneo kama hayo na kufafanua kwamba hayo ni mambo mawili tofauti.

Alisema eneo la Kahama lilikuwa la chuo cha maendeleo lililokuwa na ekari 348 na kwamba mkurugenzi aliyekuwepo aliligawa kwa wananchi, wakapewa na hati kisha akatorokea Burundi.

“Kwa sababu mkuu wa mkoa ameliomba nitalibeba nitalifanyia kazi, lakini isije kuwa ni mazoea mnavunja sheria kwa makusudi halafu mnaomba, tukikata mapori yote nchi hii haitakalika,” alisema.

Alisema Morogoro kuna matatizo makubwa kama hayo likiwamo la Kilosa ambalo kuna mtu aliyechukua mashamba ya kila aina anayetaka kujenga hoteli ili apokee watu wakafanye mambo aliyosema ya ajabu.

Kilio cha mbunge

Pia alijibu ombi la Mbunge wa Morogoro Mjini, Aziz Abood kuhusu kero ya maji alisema hilo atalibeba kwa nguvu zote na kulifanyia kazi. Alisema atamtuma waziri wa maji ili kutatua kero hiyo kutokana na umuhimu wa mkoa huo katika viwanda.

“Nafahamu kulikuwa na mpango wa kutoa maji katika bwawa la Mindu mpango ule sijui uliishia wapi? alihoji.

Mwijage anena

Awali, waziri Mwijage alisema kazi ya kujenga na kufufua viwanda nchini inaendelea na kwamba vitano vinasubiri kuzinduliwa.

Alivitaja baadhi ya viwanda vilivyokamilika vikisubiri kufunguliwa kuwa ni cha vigae kilichopo mkoani Pwani, cha nyanya (Iringa) na sabuni cha Pwani.

Kuhusu viwanda vilivyopo mkoani mwake, Dk Kebwe alisema vipo vidogo 338 vya kati 302 na vikubwa 20 ambavyo vinaendelea na uzalishaji.

Pia alisema mwekezaji wa kujenga kiwanda cha kusindika mazao jamii ya kunde kitakuwa cha kwanza Afrika Mashariki na Kati, ameshapatikana na kwamba bidhaa zitakazozalishwa zitauzwa Marekani China, India na Ujerumani.

Alisema kampeni iliyoanzishwa na mkoa huo kwa kushirikiana na Shirika la Viwanda Vidogo (Sido) na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade) wamepanga kuhamisha ujenzi wa viwanda na mpaka kufikia Desemba wanategemea kuwa viwanda vingine 300.

Akitoa taarifa ya kiwanda hicho, mkurugenzi wa kampuni ya Mansoor Industry Limited, Mansoor Shariff alisema ujenzi wake umegharimu Sh65 bilioni.