VIDEO: Magufuli,Kikwete, Polepole Mufti wawasili Karimjee kumuaga Mzee Majuto

Rais John Magufuli akitoa heshima za mwisho kwa mwili wa mwigizaji nguli wa vichekesho nchini, Mzee King Majuto wakati wa swala ya kumuombea iliyofanyika katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam leo. Picha na Ericky Boniphace

Muktasari:

Wamo pia wasanii kama Diamond Platinumz na mbunge Zainab Vullu.  

Dar es Salaam. Wakati mwili wa msanii mkongwe wa filamu nchini Amri Athuman maarufu Mzee Majuto ukiwasili viwanja vya Karimjee, viongozi wa kitaifa akiwamo Rais mstaafu Jakaya Kikwete na Rais John Magufuli  wamewasili katika viwanja  hivyo kwa ajili ya kuuaga.

Mzee Majuto alifariki dunia jana saa mbili usiku katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili alikokuwa akitibiwa.

Viongozi wengine waliohudhuria shughuli hizo za kuaga ni Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole na Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Pwani, Zainab Vullu.

Pia yupo Mufti wa Tanzania, Abubakar Zubeir na Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Musa Salum na  Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.

Baadhi ya wanakamati wamempokea Kikwete na kumpeleka katika chumba cha wageni maalumu.

Kadhalika mamia ya wasanii wamefika katika viwanja hivyo kwa ajili ya kutoa heshima za mwisho kwa msanii huyo mchekeshaji mahiri nchini.

Msanii Diamond Platinumz naye amefika viwanjani hapo.