KUELEKEA MWAKA MMOJA WA MAGUFULI: Magufuli aahidi bima ya afya, Lowassa mikataba ya madini

Rais John Magufuli

Muktasari:

Novemba 5, 2015, Rais John Magufuli atatimiza mwaka mmoja tangu aapishwe baada ya kushinda Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana. Kuelekea siku hiyo, gazeti la Mwananchi litakuwa likikuletea marudio ya habari kubwa iliyotokea siku kama ya leo mwaka jana na jinsi lilivyokuwa ikiripoti habari za kampeni hadi Uchaguzi Mkuu. Nia ni kuwakumbusha wasomaji wetu mambo mbalimbali ya Uchaguzi Mkuu ili wajue tumetoka wapi na tunaelekea wapi. Karibu katika safu hii kila siku...

Kilwa/Geita. Wagombea urais wa vyama vinavyochuana vikali, CCM na Chadema jana waliendelea na kampeni katika mikoa ya Lindi na Geita kila mmoja akinadi ilani yake kwa wananchi.

Akiwa Lindi, mgombea wa CCM, Dk John Magufuli alisema akichaguliwa, atahakikisha huduma za afya zinapatikana na ataboresha huduma za bima ya afya ili kila mwananchi apate huduma inayostahili. Alisema hayo kwa nyakati tofauti kwenye mikutano ya kampeni wilayani Kilwa. Mbali na hilo, alisema endapo atachaguliwa, ataboresha miundombinu ya Wilaya ya Kilwa ili kuvutia watalii.

Alisema atasaidia vitendea kazi vya kisasa kwa wavuvi kwa nia ya kuongeza kipato kwa wakazi na Taifa kwa ujumla.

“Mji wa Kilwa ni wa kitalii na kihistoria, mkinipa ridhaa ya kuwa rais wenu nitahakikisha narudisha hadhi yake kwa kujenga miundombinu ya kisasa zikiwamo barabara za mitaani kwa kiwango cha lami, hapa kazi tu,” alisema.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Lindi, Ali Mtopa aliwaomba wananchi kuacha kudanganyika na wapinzani kwamba ni muda wa mabadiliko ya kuiondoa CCM kuleta unafuu wa maisha.

Alisema unafuu wa maisha hauwezi kuletwa na wapinzani, bali ni CCM pekee yenye sera madhubuti ya kuwaletea wananchi mabadiliko

Lowassa na mikataba ya madini

Kwa upande wake, mgombea wa Chadema, Edward Lowassa alisema akiiangia madarakani atakachoanza kufanya ni kufumua mikataba yote ya madini ambayo haiwasaidii Watanzania na kuifuta ile inayowapendelea wageni.

Akizungumza kwenye mikutano ya kampeni Busanda na Geita jana, Lowassa alisema mikataba mingi inaonekana haiwasaidii Watanzania na jamii. Akitoa mfano, alisema majimbo hayo ni kati ya maeneo ambayo hayajaendelezwa licha ya kuwapo madini na migodi. Alisema atakuwa rafiki wa wachimbaji wadogo kwa kuwapatia vifaa vya kisasa ili kutatua tatizo la ajira.

“Vijana wana matatizo ya ajira, niliwahi kusema kuwa vijana ni bomu linalosubiri kulipuka lakini nikapingwa, sasa ninachotaka kusema ni kwamba nitaifanya JKT itoe mafunzo ya ufundi kama yanayopatikana vyuo vya Veta.”

Alisema ataongeza mara tano idadi ya vijana watakaojiunga na JKT na kwa kufanya hivyo, atakuwa ametatua tatizo la ajira kwa vijana milioni 1.5.

Huku akichagiza na kauli za mabadiliko, alisema baada ya kuapishwa, ataanza kazi kwa spidi 120 na asiyeweza kuwamo katika spidi hiyo ataachwa

Awali, wazee wa kimila wa Busanda walimsimika kuwa kiongozi wakisema wamekwishamwapisha kimila na wanasubiri kiserikali. Kiongozi wa wazee wa kimila, Petro Manyama alisema wamemsimika ili awaletee maendeleo.

Awali, Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye alisema: “Kuna watu wanawanyanyasa watumishi wa umma wanaoshabikia Chadema. “Tunaomba wawaache, kwa kuwa watumishi wana uhuru wa kushabikia upande wanaopenda.”

Mgombea ubunge wa Chadema katika jimbo hilo, Alphonce Mawazo alimwomba Lowassa kuwa akichaguliwa awakumbuke wachimbaji wadogo, wavuvi na kusaidia upatikanaji wa maji na umeme.

Akihutubia mkutano huo, Kingunge Ngombale Mwiru alimshukia Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba na Profesa Benson Bana kuwa hawana uwezo wa kuhoji uamuzi wake wa kuondoka CCM kwa kuwa ni binafsi na alishafanya uamuzi kama huo tangu enzi ya ukoloni.

“Nilifanya ukarani kwa serikali ya kikoloni, Mwalimu Nyerere akaniomba niungane naye, nikawaambia wakoloni naondoka, walinibembeleza nikaondoka kupigania Tanzania, hapo nilishawishiwa na Lowassa? Naomba waniache.”