Wednesday, June 13, 2018

Magufuli achangia Sh10 milioni ujenzi wa msikiti Bakwata

Rais  John  Magufuli, akiaga wananchi jana

Rais  John  Magufuli, akiaga wananchi jana baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Msikiti Mkuu wa Baraza Kuu la Waisalmu Tanzania (BAKWATA) unaojengwa kwa ufadhili wa Mfalme Mohamed wa Sita wa Morocco Kinondoni jijini Dar es salaam. Picha na Ikulu 

By George Njogopa, Mwananchi gnjogopa@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Rais John Magufuli amekagua maendeleo ya ujenzi wa msikiti uliopo makao makuu ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) unaojengwa kwa ufadhili wa Mfalme Mohamed VI wa Morocco na kutoa mchango.

Mbali na ukaguzi huo, Rais Magufuli alichangia Sh10 milioni kwa ajili ya ununuzi wa saruji ili kuharakisha ujenzi wa msikiti huo wenye uwezo wa kuchukua waumini zaidi ya 6,000 kwa mara moja.

Msikiti huo unajengwa Kinondoni jijini Dar es Salaam baada ya Rais Magufuli kumuomba Mfalme Mohamed VI kuwajengea Waislamu msikiti alipofanya ziara nchini Oktoba 24, 2017.

Katika ukaguzi huo, Rais alifuatana na Balozi wa Morocco nchini, Abdelilah Benryane na Mufti wa Tanzania, Aboubakary Zubeiry. Ujenzi wa msikiti huo unatarajiwa kukamilika Aprili mwakani.

Neno kwa viongozi wa dini

Rais Magufuli aliwataka viongozi wa dini kujisimamia kwa kuyasemea mambo yao na siyo kuwakaribisha watu wasiohusika wakiwamo wanasiasa.

Alisema kwa kufanya hivyo kila upande utakuwa umetimiza wajibu wake kwa kuwa watu wanaotumwa kusemea jambo fulani kwa niaba ya wengine huwa na tabia ya kuongeza chumvi kwa manufaa yao binafsi.

Rais alisema viongozi wa dini wanapaswa kuwa wasemaji wakuu wa mambo yao na si kuwaachia watu wengine ambao hawana uhusiano wowote na masuala ya kidini.

“Kwanza nikupongeze mufti unafanya kazi nzuri, katika kazi zako unazingatia maadili ya maandiko uliyoapa kuyalinda. Unasimamia kweli. Niendelee kuwaomba viongozi wa dini msiwe na wasemaji ambao si viongozi wa dini... mnapokuwa viongozi wa dini halafu mkawatumia wasemaji ambao si viongozi wa dini labda wanasiasa mtakuwa mnachanganya dini na siasa ambacho ni kitu kibaya sana,” alisema.

Akisisitiza Serikali kuendelea kushirikiana na viongozi wote wa dini, Rais Magufuli alisema kunapokuwa na wasemaji wengi katika masuala yanayohusu dini ni rahisi kupoteza mwelekeo kwa sababu wasikilizaji wanashindwa kuelewa.

“Kwa hiyo panapozungumzwa neno lolote linalohusu maadili ya dini au ushauri wowote unaohusika na dini uzungumzwe na watu wa dini wenyewe,” alisema Rais.

“Kama ni masheikh wazungumze masheikh, kama ni mufti anazungumza mufti, kama ni askofu azungumze askofu kama ni padri azungumze padri, kama ni mchungaji azungumze mchungaji, msitafute wasemaji kwa niaba ya masheikh, kwa niaba ya mapadri kwa niaba ya maaskofu mtakuwa mnatupoteza... mtakuwa Taifa mnalipeleka mahali pabaya.”

Hivi karibuni kuliibuka hali ya vuta nikuvute baada ya wabunge wa upinzani kuingilia kati suala la barua iliyodaiwa kuandikwa na ofisa wa Wizara ya Mambo ya Ndani kwenda kwa mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) iliyotaka kanisa hilo kufuta waraka wa Pasaka lililoutoa.

Waraka huo mbali ya mambo ya kiroho ulizungumzia pia masuala ya kijamii na kiuchumi likiwemo la Katiba Mpya ambao KKKT ilitakiwa kuufuta ndani ya siku 10.

Wabunge hao walitaka kanisa kutojibu barua hiyo, huku waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba akikana Serikali kuandika barua hiyo na aliamua kumsimamisha kazi msajili wa Taasisi za Dini, Maryline Komba.

Wakati huohuo, Rais Magufuli ametaka barabara itakayokarabatiwa karibu na eneo la msikiti huo ipewe jina la mkazi aliyejitambulisha kwa jina la Rashidi Masushi baada ya swali la mwananchi huyo kwa Rais kuonekana kuwa na masilahi kwa wananchi wa eneo hilo.

Masushi alipewa fursa ya kuuliza swali wakati Rais Magufuli alipowasalimu wakazi wa eneo hilo baada ya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa msikiti.

Mkazi huyo alimuomba Rais kusaidia kufanikisha ukarabati wa eneo lililopo karibu na msikiti huo akidai limekuwa likiwapa wakati mgumu wananchi kutokana na kujaa maji mara kwa mara.

“Mheshimiwa Rais hapo karibu na msikiti kuna dimbwi la maji ambalo linatufanya wakati mwingine tuwe katika wakati mgumu tunapokwenda msikitini. Kwa vile wakati fulani wewe ulikuwa mkazi wa eneo hili la Kinondoni na mimi ni mjumbe wa nyumba kumi naomba tufanyie mipango ili angalau nasi tuondokane na adha hii,” alisema Masushi.

Baada ya maelezo hayo, Rais Magufuli alisema, “Swali nzuri sana na nadhani ameuliza kwa niaba ya wananchi napenda wananchi wa namna hii, hebu tumpigie makofi Rashidi. Mkuu wa mkoa hebu chukua namba yake ili barabara hii ianze kukarabatiwa mara moja na kazi hii ifanyike kwa fedha za mfuko wa barabara....naagiza kazi ifanyike mara moja,” alisema Rais Magufuli.

Wakati mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda akibadilishana namba na Masushi, Rais Magufuli alimwita tena mkazi huyo na kumuuliza: “Hivi bwana Rashid unafanya kazi gani?”

Masushi: “Nina kibanda changu cha biashara.” Jibu hilo lilimfanya Rais Magufuli atabasamu, kisha akasema, “Njoo uchukue laki moja hapa ukaongezee biashara yako.”

Masushi alikwenda na kukabidhiwa Sh200,000. “Haya uende ukaongezee kwenye biashara yako na kuanzia sasa barabara hii itakapotengenezwa itaitwa Rashidi Masushi,” alisema Rais Magufuli.

Baada ya kupokea fedha hizo, mwananchi huyo alirejea tena sehemu aliyokuwa amesimama mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na kisha akatoa noti ya Sh10,000 na kumpa tukio ambalo lilimfanya Makonda aangue kicheko huku akirejea sehemu aliyokuwa amesimama awali.

-->