Magufuli aivunja bodi ya Tamesa

Muktasari:

Rais Magufuli ametangaza kuivunja bodi ya Tamesa ikiwa ni siku tatu zimepita tangu kutokea kwa ajali ya Kivuko cha MV Nyerere.

Dar es Salaam. Rais John Magufuli ameivunja Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Ufundi na Umeme (Tamesa) kuanzia leo.

Taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu iliyotolewa leo Jumapili Septemba 23,2018, imesema Rais Magufuli amechukua hatua hiyo baada ya kutokea kwa ajali ya kuzama kwa kivuko cha MV Nyerere.

Amesema bodi hiyo iliyo chini ya mwenyekiti wake Brigedia Jenerali Mstaafu Mhandisi Mabula Mashauri imevunjwa kuanzia leo wakati kamati ya uchunguzi kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama vikiendelea na uchunguzi wa ajali hiyo.