Magufuli akutana na trafiki Ikulu, awapongeza

Muktasari:

  • Rais John Magufuli amewapongeza askari wa usalama barabarani kwa juhudi zao za kusimamia usalama licha ya changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo

Dar es Salaam. Rais John Magufuli amewapongeza askari wa usalama barabarani kwa juhudi zao za kusimamia usalama barabarani licha ya changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo.

Kiongozi mkuu huyo wa nchi ametoa pongezi hizo leo Jumapili Septemba 23, 2018 alipokutana na kunywa chai na baadhi ya askari hao Ikulu jijini Dar es Salaam, ikiwa ni muda mfupi baada ya kutoka katika Ibada ya Jumapili iliyofanyika katika Kanisa la Mtakatifu Petro, Oysterbay.

Taarifa ya Rais kukutana na askari hao wa kikosi cha usalama barabarani imetolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa.

“Ninawapongeza trafiki wote kwa kazi mnazofanya, nafahamu mnakabiliwa na changamoto nyingi, mnafanya kazi zenu kwenye jua na mvua, wakati mwingine mnakwazwa na watumia barabara lakini mnaendelea na kazi,” amesema Rais.

“Nataka kuwatia moyo chapeni kazi, wanaovunja sheria za barabarani wachukulieni hatua, msitishwe na mtu yeyote lakini na nyie msimuonee mtu yeyote.”

Askari hao wamemshukuru Rais kwa kuwaalika Ikulu kupata nao chai ya asubuhi na kuzungumza nao, na wamemhakikishia kuwa wataendelea kuchapa kazi kwa juhudi na maarifa ili kuhakikisha usalama barabarani unazidi kuimarika.

“Tunakushukuru sana Rais kwa upendo wako kwetu, umetutia moyo sana na tunakuhakikishia tutachapa kazi kwa nguvu zetu zote,” amesema mkuu wa trafiki wa wilaya ya kipolisi ya kati, Inspekta Neema Mvungi.

Mapema leo asubuhi Rais Magufuli pia ameshiriki misa takatifu iliyoongozwa na paroko msaidizi wa Parokia ya Oysterbay, Padri Bathlomeo Bachoo.

Katika misa hiyo, yalifanyika maombi kuwaombea marehemu wote wa ajali ya kivuko cha MV Nyerere na majeruhi kupona haraka.