Saturday, August 12, 2017

Magufuli ampongeza Kenyatta

 

By Emmanuel Mtengwa, Mwananchi mmtengwa@tz.nationmedia.com

Dar es Salaam. Rais John Magufuli amemtumia salamu za pongezi Rais mteule wa Kenya, Uhuru Kenyatta kwa kuchaguliwa kuongoza nchi hiyo kwa mhula wa pili.

Rais Magufuli ametuma pongezi hizo leo Jumamosi kupitia ukurasa wake wa twitter ‘Nakupongeza Ndg.Uhuru Kenyatta kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Kenya kwa kipindi kingine. Nakutakia mafanikio mema’ ameandika Rais Magufuli

Matokeo ya urais yalitangazwa jana saa nne usiku ambapo Rais Kenyatta alipata kura 8, 203,290 sawa na asilimia  54.27 huku Raila Odinga aliyegombea kwa mwamvuli wa muungano wa Nasa akishika nafasi ya pili kwa kupata kura 6, 762,224 sawa na asilimia 44.74.

Hata hivyo, marais wengine wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) walituma salamu zao za pongezi muda mfupi baada ya matokeo hayo kutangazwa na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Wafula Chebukati.

Wakauu hao wa EAC waliotuma salamu zao za pongezi kupitia kurasa zao za twitter ni pamoja na Rais wa Rwanda, Paul Kagame ambaye amechaguliwa hivi karibuni kuongoza nchi hiyo kwa mhula wa tatu.

Wengine ni Rais wa Uganda, Yoweri Museveni‏ na Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza‏.

-->