Magufuli amtaka balozi kuwaleta wawekezaji

Muktasari:

Rais John Magufuli amemueleza Balozi wa Georgia nchini Tanzania, Zurab Dvalishivili  kuwaleta wawekezaji hasa katika sekta ya viwanda

 

Dar es Salaam. Rais John Magufuli amemueleza Balozi wa Georgia nchini, Zurab Dvalishivili kuwaleta wawekezaji hasa katika sekta ya viwanda.

Pia  amemueleza Balozi wa Japan nchini, Shinichi Goto kwamba ana amini ushirikiano wa nchi hizo mbili utakuzwa zaidi kwa kuhakikisha miradi inayoendelea inakwenda vizuri na miradi mipya inaongezeka.

Ameyasema hayo Leo Oktoba 19, 2018 alipokuwa akipokea hati za utambulisho za mabalozi hao walioteuliwa kuziwakilisha nchi zao hapa Tanzania.

Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa imesema Goto makazi yake yatakuwa jijini Dar es Salaam na Dvalishivili makazi yake ni  Addis Ababa Ethiopia.

Rais Magufuli amesema Tanzania itaendeleza kukuza zaidi uhusiano wake na nchi hizo hasa kushirikiana katika uwekezaji, biashara, utalii na ujenzi wa miundombinu.

“Tanzania na Japan zimeshirikiana katika utekelezaji wa miradi mingi ya ujenzi wa miundombinu na utoaji wa huduma za kijamii, naamini ushirikiano huo utakuzwa zaidi kwa kuhakikisha miradi inayoendelea inakwenda vizuri na miradi mipya inaongezeka, ” amesema Rais Magufuli.

Mabalozi hao wameahidi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Tanzania ili kuendeleza na kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano kati ya nchi zao na Tanzania.