Magufuli asema hawezi kutenga fedha za mchakato wa Katiba Mpya

Muktasari:

Wakati mchakato wa Katiba Mpya ukiwa umesimama na haijulikani utaendelea lini, Rais John Magufuli amesema hawezi kutenga fedha kuendelea na mchakato huo, ni vyema fedha hizo zikatumika katika ujenzi wa reli ya kisasa.


Dar es Salaam. Rais John Magufuli amesema hawezi kutenga fedha kwa ajili ya mchakato wa Katiba licha ya kutambua kiu ya wananchi kupata Katiba Mpya.

Akizungumza katika kongamano la uchumi na siasa lililofanyikia Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM) leo Alhamisi Novemba Mosi, 2018, Rais Magufuli amesema kutenga fedha hizo ni sawa na kuwapeleka watu kulipana posho, ni vyema fedha hizo zikatumika katika ujenzi wa reli ya kisasa (SGR).

Mchakato wa Katiba Mpya ulizinduliwa  na Rais mstaafu Jakaya Kikwete mwishoni mwa mwaka 2011 alipounda Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba.

Hata hivyo, mchakato huo uliishia kwenye Bunge Maalum la Katiba ambalo licha ya kupitisha Katiba Inayopendekezwa ambayo haijapigiwa kura ya maoni hadi leo, baadhi ya vyama vya upinzani vilijitoa na kuunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), na kupinga mchakato huo kwa maelezo kuwa alivurugwa na CCM.

Katika ufafanuzi wake wa leo Rais Magufuli amesema wanaotaka kusaidia kutoa fedha kwa ajili ya mchakato huo wazilete zikatumike katika miradi ya maji na barabara.

"Sasa sifahamu baada ya  rasimu ya Jaji Joseph Warioba miaka minne iliyopita  tunaendelea na hiyo rasimu au tunakwenda kuanza upya. Badala ya kulumbana kwa hayo ya Katiba bora tufanye kazi sasa "amesema Magufuli.

Amesema kuna nchi zina katiba za miaka mingi na wamezifanyia marekebisho.

"Lakini watu wameng’ang’ania katiba mpya utadhani ndiyo suluhisho la matatizo yote," amesema Magufuli na kusisitiza kuwa hawazuii wanaotoa maoni yao, lakini mtazamo wake ni Tanzania kwanza.