Magufuli ataja sababu kusitisha uingizaji sukari ya Uganda

Rais John Magufuli akipeana mkono na mgeni wake, Rais Yoweri Museveni wa Uganda walipokutana na kufanya mazungumzo Ikulu jijini Dar es Salaam jana. Museveni alikuja nchini katika ziara ya siku moja. Picha na Anthony Siame

Muktasari:

  • Februari, Rais wa Uganda, Yoweri Museveni alimsihi Rais Magufuli kuwahimiza wafanyabiashara wa Tanzania kununua kwa wingi sukari kutoka Taifa hilo kwa sababu ipo ya kutosha na ziada

Dar es Salaam. Rais John Magufuli ametaja sababu za kuzuiwa kuingia nchini sukari kutoka Uganda akisema hatua hiyo ilitokana na baadhi ya watu kuleta sukari isiyozalishwa nchini humo.

Februari, Rais wa Uganda, Yoweri Museveni alimsihi Rais Magufuli kuwahimiza wafanyabiashara wa Tanzania kununua kwa wingi sukari kutoka Taifa hilo kwa sababu ipo ya kutosha na ziada.

Akizungumza Ikulu mjini Entebbe, Uganda na Rais Magufuli alikokwenda kuhudhuria mkutano wa 19 wa wakuu wa nchi wanachana wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Museveni alisema Taifa hilo limekuwa likizalisha ziada ya sukari, hivyo itakuwa vyema iwapo atawahimiza wafanyabiashara kuchangamkia fursa hiyo.

Rais Magufuli alikubaliana na wazo hilo na kusema litasaidia kukabiliana na changamoto ya upungufu wa sukari nchini.

Hata hivyo, hivi karibuni Tanzania ilisimamisha uingizaji wa sukari kutoka Uganda, jambo lililoibua malalamiko kutoka kwa wafanyabiashara wa nchi hiyo.

Dk Magufuli akizungumza Ikulu jijini Dar es Salaam, jana, alikokutana na Museveni aliyefanya ziara ya siku moja nchini, alisema Serikali ililazimika kusitisha uigizaji wa sukari baada ya kubaini kiwango kikubwa hakizalishwi Uganda.

Mkutano wa Rais Magufuli na Museveni ulirushwa moja kwa moja na kituo cha televisheni cha TBC1.

Rais alisema baadhi ya wafanyabiashara kutoka nje ya Uganda walikuwa wakipenyeza sukari nchini humo na baadaye kuisafirisha hadi Tanzania, jambo alilosema ni hatari kwa viwanda vya ndani.

“Utandawazi katika biashara ni mzuri lakini pia tunatakiwa tuangalie vizuri. Nilizungumza wakati fulani kwamba tunahitaji sukari inayotengenezwa kutoka Uganda ije Tanzania na tungependa bidhaa kutoka Tanzania ziende Uganda, ziende Kenya ziende mahali pengine,” alisema Dk Magufuli.

Alisema Tanzania imekuwa ikipata bidhaa nyingi kutoka Uganda akitoa mfano mwaka jana ilipokea mahindi kutoka Taifa hilo, lakini katika sukari ilijitokeza changamoto ya namna ya uingizaji.

Rais Magufuli alisema iwapo kutajitokeza mahitaji ya sukari, kiwango kinachohitajika kinapaswa kuangaliwa kwa umakini ili kuepuka tabia ya wajanja wachache kuzigeuza nchi hizo kuwa jalala la kutupia bidhaa.

Pia, alisema mwenendo wa namna hiyo ukiachwa uendelee unaweza kusababisha athari kubwa kwa viwanda vya ndani.

“Katika viwanda vingi vilivyopo Tanzania sasa hivi vina sukari nyingi tu, tulikuwa tunaona kwa mfano Kagera Sugar magodauni yote yamejaa sukari, nyingine wanaipaki nje ni kwa sababu palikuwa na ambayo iliingizwa humu kinyume cha sheria. Kwa taarifa nilizonazo za jana na juzi kule Sirari yanaingia malori zaidi ya 20 kila siku ya sukari za magendo, sasa athari tunayoipata Tanzania vivyo hivyo inaipata Uganda kwa sukari inayotoka nje kuja kuua viwanda,” alisema. Tanzania huwa na upungufu wa zaidi ya tani 100,000 ya sukari kwa mwaka kiwango ambacho huagizwa kutoka nje.

Usafiri wa reli

Kwa upande wake, Rais Museveni alisema amevutiwa na hatua ya Dk Magufuli kufufua mpango wa usafiri wa reli kutoka Dar es Salaam kwenda Mwanza hadi Jinja nchini Uganda.

Alisema usafiri huo mbali ya kurahisisha biashara, pia utakuwa wenye gharama nafuu na kupunguza uharibifu wa barabara.

“Unajua tamaa inaua akili, wafanyabiashara kwa kusafirisha bidhaa kwa kutumia malori wanapata faida sana, lakini gharama yake kubwa na wakati huohuo barabara zinaendelea kuharibika,” alisema Rais Museveni.