Monday, January 15, 2018

Magufuli ataja sababu za kumuunga mkono Kagame kuongoza AU

By Peter Elias, Mwananchi pelias@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Rais John Magufuli amesema Rais Paul Kagame wa Rwanda anafaa kuongoza Umoja wa Afrika (AU) kwa sababu ya historia yake na hivyo anazifahamu changamoto zinazolikabili bara hili.

Rais Magufuli alisema hayo jana Ikulu wakati Kagame alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja, ikiwa ni mara yake ya pili kufanya ziara tangu Rais Magufuli alipoapishwa. Alifanya ziara kwa mara ya kwanza Julai Mosi, 2016.

Magufuli alimwaga sifa hizo akianzia matatizo yaliyoibuka nchini Libya baada ya kiongozi wake wa kijeshi, Muamar Gadaffi kuondolewa madarakani kwa vurugu licha ya kuliongoza taifa hilo vizuri kiuchumi.

“Baada ya kiongozi wa Libya kuondoka, na nyinyi nyote mnajua, matokeo yake ni haya. Na haya ndiyo ya ukweli na utabaki kuwa ukweli,” alisema Rais Magufuli katika hafla fupi iliyofanyika Ikulu jana.

“Nina uhakika Mheshimiwa Kagame atakapokuwa mwenyekiti wetu Afrika, atayaadress (atayashughulikia haya), atayaadress vizuri masuala ya migogoro miongoni mwa nchi za Afrika, atayaaddress vizuri masuala ya ukoloni mamboleo unaoweza kuletwa na mtu yeyote kutoka nje akasababisha matatizo kwa Waafrika.

“Mheshimiwa Kagame hadi kufikia urais anafahamu shida za wananchi wa Rwanda; anajua historia ya Rwanda ilitokotoka hadi ikatokea genocide (mauaji ya watu wengi). Anafahamu mateso ya Wanyarwanda; anafahamu mateso yanayoweza kuletwa na mtu hata mmoja tu, inawezekana ikawa ni media kwa kutangaza au kuandika kitu cha ovyo kikaleta multiplying effect.”

Alisema ndio maana anaamini kutokana na mchango wake kwa Afrika na kwa sababu ni mwanamapinduzi mzuri, uzoefu wake utasaidia maendeleo ya Afrika.

“Rais Kagame ni mwanamapinduzi wa kweli wa Afrika, ameishi maisha ya Kiafrika, maisha ya mateso tangu akiwa kijana; ameishi kwenye nchi za ugenini kama mkimbizi, anayafahamu mateso ya kijana,” alisema.

“Kwa hiyo kwa yale maisha aliyoyaishi kama mkimbizi, kama kijana, nina uhakika ataleta mageuzi makubwa Rwanda ambayo ameshaanza kuyaleta, lakini ataleta mageuzi makubwa Afrika.”

Alisema Tanzania inamuunga mkono Rais Kagame kwa nguvu zote ili kuwepo kwa mabadiliko ya kiuchumi kwa Waafrika wote hasa kwa vijana ambao ndiyo nguvu kazi kubwa katika bara hili.

Rais Magufuli pia alizungumzia miradi ambayo Serikali inaendelea kuitekeleza, akisema yote inatengeneza ajira na kuwataka vijana kutumia fursa hizo.

Pia alisema wamekubaliana kuanza ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) mwaka huu itakayotoka Isaka mpaka Kigali, Rwanda ili kurahisisha biashara baina ya nchi hizi mbili.

Kiongozi huyo alisema wamekubaliana kwamba mawaziri wa pande zote mbili wanaohusika na miundombinu wakutane wiki ijayo kujadili namna ya kugharamia mradi huo ili mwaka huu waweke jiwe la msingi kuzindua mradi huo.

Kwa upande wake, Rais Kagame alimshukuru Rais Magufuli kwa ahadi ya ushirikiano aliyompa atakapoanza kuongoza Umoja wa Afrika (AU) na kwamba anafurahi kufanya kazi na Rais Magufuli pamoja na marais wengine.

Alisema anategemea kuleta maendeleo kwa Waafrika wote na atakuwa anawasiliana mara kwa mara na Rais Magufuli na kumuomba ushauri kuhusu nchi zao. Alisema wanataka kuona wafanyabiashara wao wanafanya biashara kwa ufanisi.

Kuhusu tatizo la vijana wa Afrika kukimbilia Ulaya, Rais Kagame alisema itakuwa rahisi kukabiliana na tatizo hilo endapo nchi zote za Afrika zitafanya kazi pamoja wakati nchi mojamoja zikiendelea kutimiza wajibu wao kwa vijana.

Alisisitiza kwamba jukumu kubwa linabaki kwa vijana wenyewe ambao wanatakiwa kutumia fursa zinazopatikana kujiletea maendeleo. Alisema serikali zina wajibu wa kuwapatia elimu na kuwajengea mazingira wezeshi.

Mizigo ya Rwanda yaongezeka bandarini

Wakati huohuo, Rais John Magufuli alisema kiwango cha mizigo inayokwenda Rwanda kupitia bandari ya Dar es Salaam kimeongezeka mpaka kufikia tani 950,000 mwaka jana licha ya biashara katika ya mataifa hayo kupanda na kushuka kila mwaka.

Hata hivyo, amesema amekubaliana na Rais wa Rwanda Paul Kagame ambayo yuko nchini kwa ziara ya siku moja kwamba watahamasisha wafanyabiashara wa Rwanda na Tanzania kushirikiana pamoja na kujenga mazingira mazuri ya kibiashara.

Rais Magufuli alisema biashara kati ya mataifa hayo mawili imekuwa ikipanda na kushuka na serikali zao zimepanga kupandisha biashara kwa kujenga mazingira wezeshi ikiwemo mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Isaka (Tanzania) mpaka Rwanda.

Alibainisha kwamba mwaka 2011, biashara kati ya Rwanda na Tanzania ilikuwa na thamani ya Sh106.5 bilioni; mwaka 2012 ilishuka mpaka Sh27.3 bilioni; mwaka 2013 – Sh132.2 bilioni; mwaka 2014 – Sh64.45 bilioni na mwaka 2015 ilikuwa Sh83.95 bilioni.

“Sasa unaweza ukaona trend, kwamba biashara imekuwa inapanda na kushuka. Sasa katika mazungumzo yetu tumekubaliana kwamba biashara kati ya nchi hizi mbili lazima ianze kupanda na kupanda kwanza kunatokana na wananchi wa nchi hizi mbili wakubali kufanya biashara lakini jukumu jingine kubwa la serikali ni kuhakikisha kwamba serikali zote mbili inatengeneza mazingira mazuri ya kufanya biashara,” alisema Rais Magufuli.

-->