Magufuli ataka ‘flyover’ ya Ubungo iiishe kabla ya miezi 30

Muktasari:

Barabara hiyo ya juu (flyover) itajengwa na mkandarasi kampuni ya China ya CCECC kwa Sh188.7 bilioni, kati ya hizo Benki ya Dunia (WB) itatoa Sh186.8 bilioni kwa ajili ya ujenzi na usanifu na Sh1.9 bilioni zitatolewa na Serikali kwa ajili ya kulipa fidia.

Dar es Salaam. Rais John Magufuli ametaka ujenzi wa barabara ya juu (Ubungo Interchange) katika makutano ya barabara Ubungo ukamilike mapema kabla ya miezi 30, muda ambao mkandarasi amepewa katika mkataba wake na Serikali.

Barabara hiyo ya juu (flyover) itajengwa na mkandarasi kampuni ya China ya CCECC kwa Sh188.7 bilioni, kati ya hizo Benki ya Dunia (WB) itatoa Sh186.8 bilioni kwa ajili ya ujenzi na usanifu na Sh1.9 bilioni zitatolewa na Serikali kwa ajili ya kulipa fidia.

Ujenzi huo ambao ni mkopo nafuu kutoka WB, ulizinduliwa rasmi jana na Rais Magufuli akiwa na Rais wa WB, Dk Jim Yong Kim na makubaliano ni kwamba ukamilike Septemba 2019.

Rais Magufuli na Dk Kim waliwasili eneo la makutano ya Ubungo wakiwa wamepanda basi liendalo haraka ikiwa ni ishara ya kutambua mchango wa WB katika ujenzi wa awamu ya kwanza ya Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT).

Akizungumza kabla ya uzinduzi huo, Rais Magufuli alisisitiza kwamba hakuna haja ya mkandarasi kuchelewesha ujenzi wa barabara hiyo ya juu kwa sababu fedha zipo na ikiwezekana wamalize ujenzi huo ndani ya miezi 20.

“Sioni sababu ya mradi huu kufika miezi 30 kwa sababu kuna usiku na mchana, tena ni vizuri kufanya kazi usiku kwa sababu hakuna magari yanayopitapita na kuleta usumbufu. Wanaweza kukamilisha mradi huu hata kwa miezi 12,” alisema Rais Magufuli na kushangiliwa na wananchi.

Aliwataka wananchi walipe kodi ili Serikali iweze kulipa mkopo iliopata kutoka WB na kutekeleza miradi mingine ya maendeleo.

Alisema, “bahati nzuri nchi yetu inakopesheka na mikopo hiyo ina riba nafuu kuliko mikopo mingine. Kwa mfano, interest (riba) ya mkopo huu kutoka Benki ya Dunia ni asilimia 0.5 tofauti na mikopo mingine ambayo riba yake inafika mpaka asilimia 28.

“Hakuna hata senti tano itakayopotea na atakayepoteza atatumbuliwa. Serikali ya awamu ya tano imejipanga kushirikiana na sekta binafsi katika kuwaletea maendeleo wananchi, ndiyo maana leo (jana) tuko hapa na Rais wa WB.”

Uzinduzi huo uliambatana na utiaji saini wa mikataba mitatu iliyosainiwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango na Mkurugenzi wa Benki ya Dunia nchini, Bella Bird mbele ya Rais Magufuli na Dk Kim.

Mikataba hiyo itakayogharimu zaidi ya Sh1.74 trilioni ni ya uboreshaji wa usafiri katika jiji la Dar es Salaam, usambazaji maji na wa kuboresha miji kadhaa ikiwamo Arusha, Dodoma, Mbeya na Mtwara.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa alisema mradi huo wa barabara za juu Ubungo utakuwa ni ukombozi kwa wakazi wa Dar es Salaam kwa sababu utapunguza foleni katika mkoa huo.

Aliwataka wananchi kutumia fursa hiyo ya ujenzi kujipatia ajira lakini pia kuitunza miundombinu hiyo itakapokamilika. Alisisitiza kwamba barabara hizo pamoja na mradi wa BRT zitakuwa ni sehemu ya suluhisho la foleni katika jiji la Dar es Salaam.

“Mradi wa mabasi yaendayo haraka umeleta mageuzi makubwa katika usafiri wa hapa jijini. Kwa ufadhili wa Benki ya Dunia, tutaendelea kujenga awamu nyingine zijazo ili kuwaondolea wananchi adha ya foleni barabarani,” alisema.

Dk Kim alisema uongozi ni jambo muhimu kwa maendeleo ya Taifa kwa sababu miradi inapokuja inakutana na rasilimali za ndani, kama hakuna uongozi mzuri hakuna maendeleo yanayoweza kupatikana.

Alisema WB imekuwa ikikosolewa kwa kuangalia Pato la Taifa la Ndani (GDP) katika kupima maendeleo ya Taifa badala ya kuangalia pato la wananchi. Alimpongeza Rais Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya hasa katika kupambana na ufisadi.

Alisema ujenzi wa barabara hiyo ya juu ni matokeo ya ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi na kwamba WB itaendelea kuunga mkono jitihada za Tanzania kuwa nchi yenye uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

“Sisi WB hatutawaacha, tutashirikiana katika miradi mbalimbali ya maendeleo. Ninamwamini sana Rais Magufuli, nitakuja tena Tanzania kuangalia maendeleo yaliyofikiwa,” alisema Dk Kim ambaye benki yake imekuwa ikifadhili miradi mbalimbali ya maendeleo.

Mbali na ujenzi wa barabara za juu za Ubungo, miradi mingine yenye lengo la kupunguza foleni jijini Dar es Salaam ni pamoja na ujenzi wa barabara ya juu ya Tazara, daraja la Kigamboni, barabara ya Msata na mradi wa mabasi yaendayo haraka.