Magufuli atamba CCM itatawala milele

Muktasari:

Ametoa kauli hiyo leo katika uzinduzi wa Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Julius Nyerere Kibaha mkoani Pwani

Dar es Salaam. Rais John Magufuli amezindua Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Julius Nyerere na kubainisha kuwa Chama cha Mapinduzi (CCM) kitaendelea kutawala milele kwa kuwa hakina mbadala.

Akizungumza leo Jumatatu Julai 16, 2018 katika uzinduzi  wa ujenzi wa chuo hicho Kibaha mkoani Pwani, kiongozi mkuu huyo wa nchi amesema chuo hicho ni moja ya sababu ya CCM kuimarika kwa kuwa kitazalisha viongozi wazuri.

“CCM ni chama tawala na kitaendelea kutawala milele na milele, wanaohangaika watapata tabu siku zote. Chama hiki kipo na kitaendelea kuwepo na kitaendelea kuleta maendeleo kwa ajili ya Watanzania. Hakuna mbadala ni CCM hadi milele,” amesema.

“Wanachama wa CCM tembeeni kifua mbele tumeamua kuleta Tanzania mpya inayowapigania wananchi  hasa wanyonge ili waweze kushiriki katika maendeleo.”

Rais Magufuli ameviomba vyama sita vya ukombozi kusini mwa Afrika vinavyoshirikiana kujenga chuo hicho, kufikiria kupanua wigo wa kuweka masomo mengine ya masuala ya maendeleo, badala ya kufundisha itikadi pekee.

Pia amevitaka kuwakaribisha wanachama wa vyama vingine wenye mrengo unaofanana na vyama hivyo,  kujiunga na kujifunza kozi mbalimbali zitakazotolewa katika chuo hicho.

 “Makatibu wa vyama hivi sita wahahakikishe wanakamilisha taratibu zote mapema ili majengo yakikamilika, mafunzo hayo yaweze kuanza mapema, pia mkandarasi akamilishe mapema na awashirikishe wananchi katika ujenzi huo ili nao waweze kunufaika,” amesema

Amebainisha kuwa chuo hicho kitasaidia  kuzalisha viongozi wenye sifa wanaotambua itikadi,  kwamba vyama vina misingi ya kiitikadi inayofanana.

Amesema uanzishwaji wa chuo hicho ni  mwelekeo mwingine wa kushirikiana kwenye masuala ya kiuchumi na kisiasa, kwamba kitatoa mchango mkubwa katika mwelekeo huo.

Vyama vinavyomiliki chuo hicho ambavyo baadhi ya viongozi wake wamehudhuria uzinduzi huo ni  ZANU-PF cha Zimbabwe, MPLA cha Angola, Frelimo (Msumbiji), MPLA (Angola), ANC (Afrika Kusini) na  Swapo (Namibia).