Magufuli atuma salamu za rambi rambi vifo vya watu 18

Rais John Magufuli

Muktasari:

Ajali hiyo ilitokea Majira ya saa moja jioni baada ya gari dogo aina ya Noah lililokuwa limebeba abiria 21 kugongana uso kwa uso na lori na kusababisha vifo vya watu 18 na wengine watatu kujeruhiwa.

Dar es Salaam. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  John Pombe Magufuli, amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Zainabu Telack kufuatia vifo vya watu 18 vilivyosababishwa na ajali ya barabarani katika kijiji cha Salala Kilichopo katika Wilaya ya Shinyanga Vijijini Mkoani Shinyanga juzi Novemba 6.

Ajali hiyo ilitokea Majira ya saa moja jioni baada ya gari dogo aina ya Noah lililokuwa limebeba abiria 21 kugongana uso kwa uso na lori na kusababisha vifo vya watu 18 na wengine watatu kujeruhiwa.

Katika salamu hizo Rais Magufuli ameelezea kusikitishwa na ajali za barabarani zinazoendelea kutokea na ametaka vyombo vinavyohusika na wadau wa usalama barabarani kushirikiana kukabiliana na ajali hizo.

"Ni jambo linaloumiza na kusikitisha sana kupoteza idadi kubwa ya watu namna hii, nakuomba Ndugu Mkuu wa Mkoa Shinyanga  Zainab Telack unifikishie pole nyingi kwa familia za Marehemu wote, ndugu, jamaa na marafiki waliopoteza jamaa zao na uwaambie tupo pamoja katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo," amesema Rais Magufuli.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein kufuatia kifo cha Mwenyekiti Mstaafu wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar Jaji Zubeir Juma Mzee kilichotokea jana tarehe 07 Novemba, 2016 Mjini Unguja.

Sambamba na salamu hizo, Rais Magufuli pia amemtumia salamu za rambirambi Dk Ali Shein ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Zanzibar kufuatia kifo cha Naibu Katibu Mkuu Mstaafu wa CCM, Saleh Ramadhan Ferouz kilichotokea usiku wa kuamkia leo tarehe 08 Novemba, 2016 Mjini Unguja.

"Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein, nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za viongozi wetu wastaafu waliotangulia mbele za haki hapo jana, tutawakumbuka kwa mchango wao mkubwa kwa Zanzibar na Taifa letu kwa ujumla kwa kuwa katika kipindi chao cha uongozi walijitahidi kutimiza wajibu wao na kuleta manufaa kwa Taifa" alisema

Rais Magufuli amewaombea marehemu wote wapumzishwe mahali pema peponi. Amina